Zari Afichua Mambo Mazito Yanayomhusu Diamond - BongoSwaggz.Com

Advert

Breaking News

Zari Afichua Mambo Mazito Yanayomhusu Diamond

Jana tulianza kuchapisha mfululizo wa simulizi ya mwanadada Zarina Hassan maarufu kama Zari the bosslady, ambapo alieleza mambo mengi wakati akifanya mahojiano maalumu jijini Johanesburg, Afrika Kusini.

Ameeleza mengi kuhusiana na walivyoanza kujirusha na Diamond hadi kupata watoto, Nillan na Tiffah. Pia, alifunguka maisha yake na mumewe, marehemu Ivan Ssemwanga na wapenzi wake wengine ambao, aliwahi kuwa nao kwenye maisha yake.

Lakini, unajua kuwa Zari na Ivan hawakuwahi kufunga ndoa licha ya kuvalishana pete ya uchumba na kupata watoto watatu pamoja? Na je, unafahamu kabla ya kuwa na Diamond alikuwa akitoka na mwanaume, ambaye ni wa kawaida tu. Endelea na simulizi hii.

“Ivan alikuwa na mambo mengi na hakunipa heshima iliyostahili. Mimi ni mwanamke ninayethamini zaidi utu na heshima. Mambo ya pesa, magari na dhahabu ni nyongeza tu lakini kitu cha muhimu zaidi ni mapenzi,” anasema Zari.

Zari anafichukua kitu ambacho Watanzania wengi hawakifahamu. Baada ya kuachana na Ivan hakuja moja kwa moja kwa Diamond na badala yake aliwahi kuwa katika uhusiano na mwanaume wa kawaida kabisa wa jijini Kampala.

“Huyo mwanaume wala hakuwa tajiri. Hakunipa chochote na ungeweza kuona kuwa alikuwa ni mshamba tu. Huwa sijali pesa wala umaarufu katika mapenzi,” anaongeza Zari.

“Na hata nilipokutana na Nassib nikasema basi acha tutulie tu. Kuna mambo mengi ambayo nimefanya naye, lakini huwa nachukia kila nikikumbuka jinsi ambavyo baadaye amekuja kunigeuka na kufanya mambo ya kipuuzi ambayo yamenishushia heshima yangu na yake pia. Hata hivyo, sina tatizo naye.”

Zari anakiri maisha yake na ya Diamond ya leo hayakuanza kama yalivyokuwa sasa. Anakumbuka jinsi alivyokuwa na mchango mkubwa katika maisha ya zamani ya Diamond kitu ambacho watu wengi huwa hawakifahamu.

“Mimi niliamua kuja kuishi Tanzania kwa sababu Nassib alikuwa na shughuli nyingi Tanzania. Wakati nimeamua kuja kuishi kabisa nakumbuka nilikuwa na mimba kubwa ya Tiffah. Kwanza nikatoa mchango wangu kumalizia nyumba ya Madale, baada ya hapo nikiwa na tumbo langu tukazunguka sana katika maduka makubwa ya hapa Sandton kutafuta fenicha ambazo akilini nilikuwa najiwekea kuwa nataka kuishi maisha yale yale ambayo nilikuwa Afrika Kusini.”

“Sikutaka mwanangu azaliwe halafu tuishi katika nyumba za kawaida kwa hiyo nilipambana kuhakikisha tunamalizia nyumba ya Madale kwa ajili ya mtoto kuishi katika mazingira mazuri. Nilikuwa naishi maisha mazuri Afrika Kusini na nilitaka mazingira kama yale pia Tanzania.”

“Leo unaposoma mitandaoni kuwa kuna wasichana wanakwenda pale na kupiga picha wakati sipo unajiuliza, hiki ni kitu gani jamani? Nyumbani pale Madale palipaswa kuheshimika sana. Unaweza kufanya ujinga wako nje lakini sio katika sehemu ambayo nilishiriki kwa kiasi kikubwa kuifanya iwe ilivyo.”

Zari hataki kwenda ndani zaidi kuzungumzia kama kuna pesa zozote alitoa katika ujenzi wa nyumba ya Madale au fenicha zilizoingia ndani, lakini anaamini kwa kiasi kikubwa alileta mabadiliko ya kimaisha kwa Diamond.

“Kabla ya nyumba ya Madale hatukuwa na mbele wala nyuma. Yes, Nassib ni staa lakini alikuwa anahaha tu. Sikutaka watoto wangu waone tofauti kati ya maisha ya Afrika Kusini na maisha ya Tanzania ndio maana na mimi nilijitahidi.”

Baada ya kupata watoto wawili na Diamond, Zari anaamini alipambana kufa na kupona kuhakikisha kwamba, wanaishi maisha ya amani lakini ilishindikana. Pigo la mwisho lilikuja wakati Diamond alipozaa na mwanamke mwingine, Hamis Mobetto wakati akiwa bado ndani ya penzi lao huku wakilala kitanda kimoja.

Zari hawezi kumtaja Hamisa kwa jina lakini anakuwa makini kuelezea jinsi ambavyo Diamond alichemka zaidi kwa kwenda katika redio na kuzungumzia habari hiyo bila hata ya kujaribu kumhusisha wakiwa chumbani pamoja.

“Nilisikia tu Baba Tee amekwenda redioni kukiri. Wakati mwingine sina shida mwanaume kuzaa nje. Wanaume duniani kote ndivyo walivyo. Huwezi kumzuia mwanaume kutoka nje. Na inapotokea ishu ya mwanaume kuzaa nje, basi kama mwanaume ana akili anakuja kwako na kukwambia ‘sikia Mama Tee, nimezaa nje kwa bahati mbaya na mwanamke huyu’. Hapo kazi yangu kama mwanamke ni kuimaliza habari hii kwa kumkingia kifua mwanaume wangu. Sio kwamba akatae mtoto, hapana, jamii inataka kujua reaction yangu dhidi ya mpenzi wangu. Kama nikionekana kutojali basi jamii inapoa. Sasa unakwenda redioni bila ya kuniambia kilichotokea. Unataka na mimi nisikie redioni? Hapana sio sawa,” anasema Zari kwa uchungu.

Siku zinakatika bila ya Zari kuonyesha kurudiana na Diamond. Mmoja kati ya watu wa karibu wa Diamond, Babu Tale ambaye pia ni meneja wake inasemekana alitumwa kwenda jijini Pretoria kwa ajili ya kuangalia uwezekano wa kurudisha penzi hilo. Zari hafichi kwamba alibembelezwa sana kurudiana na Diamond.

Unafahamu uamuzi wake kuhusiana na kurudiana na Diamond? Je, unafahamu Babu Tale alichoambiwa kufikisha kwa Diamond? Fuatilia kesho Jumamosi kujua kwa undani zaidi.

-Mwananchi

Download App Yetu MPYA  >> BOFYA HAPA << Tukutumie Habari na Burudani Zote FASTA Kila Siku !

No comments

TOA MAONI YAKO HAPO CHINI.