Zari Aeleza Alivyoombwa Msamaha na Diamond Platnumz - BongoSwaggz.Com

Advert

Breaking News

Zari Aeleza Alivyoombwa Msamaha na Diamond Platnumz

MREMBO na mjasiriamali, Zarina Hassan ama ukipenda muite Zari the bosslady, amefunguka mengi kuhusiana na maisha yake na wanaume ambao aliwapa moyo wake hadi kuwazalia watoto, Ivan na Diamond. Lakini, baadaye ndio ikawa kama ulivyosikia na sasa ameamua kufungua moyo wake na kuzungumza mambo mazito.
Jana katika simulizi yake alifichua jinsi alivyoombwa sana msamaha ili kurudiana na Diamond na leo anafichua msimamo wake na majibu aliyowapa watu waliotumwa kuzungumza naye akiwemo Meneja wa Diamond, Babu Tale aliyesafiri hadi Afrika Kusini kwa shughuli hiyo. Endelea naye katika sehemu hii ya mwisho ya simulizi yake...
“Ni kweli, lakini nilisema hapana. Hata hivyo, Babu Tale ambaye pia ni rafiki yangu alitaka turudishe uhusiano wetu mzuri kwa ajili ya watoto. Hiki ni kitu cha msingi. Sikuona ubaya katika jambo hilo. Lakini mambo ya mapenzi hapana tena,” anasema Zari.
Nyuma ya safari ya Babu Tale kwenda Pretoria, Zari anashangaa kwamba ilitumika nguvu nyingi lakini watu haohao wa karibu walipaswa kumuonya Diamond wakati anafanya mambo yake kwa sababu anaamini walifahamu kila kitu.
“Wangeweza kumwambia Nassib aachane na mambo aliyokuwa anayafanya. Kujaribu kufufua penzi sasa hivi ni ngumu sana, wamechelewa. Nawaheshimu sana na ndio maana Babu Tale alikuja nikamkaribisha vizuri. Sina ubaya na mtu yeyote, hata ndugu zake Nassib.”
Kama vile haitoshi, baada ya Babu Tale kuondoka Pretoria, siku chache zilizofuata zilivuja picha za Diamond akiwa anacheza na watoto wake katika nyumba yake na Zari palepale Pretoria.
“Ndio Baba Tee alikuja kuwaona watoto wake. Alilala katika chumba kingine mimi nikalala chumbani kwangu. Tulizungumza namna ya kuwa karibu kwa ajili ya watoto wake. Hawa ni watoto wake na haiwezi kubadilika kamwe. Anawapenda watoto wake which is good na pia watoto wake wanampenda sana,” anasema Zari.
Nini kinafuata katika maisha ya Zari? Ana uhusiano wowote wa kimapenzi na mwanaume mwingine?
“Hapana. Sina uhusiano wowote ule. Kwa sasa hayo mambo nimeyaweka kando. Nawalea watoto wangu. Hauwezi kuamini mpaka sasa hivi sijarudi nyumbani sio kawaida yangu. Kina Tiffah lazima wataniulizia kwa sababu sio kawaida yangu. Mimi ikifika saa kumi na moja jioni tayari nipo nyumbani. Napika na kuwaandalia chakula wanangu kama mama mwingine yeyote yule,” anasema Zari.
Vipi kuhusu maisha yake ya kazi binafsi?
“Kwa sasa naandaa shoo yangu ya TV. Itakuwa shoo ambayo inazungumzia maisha yangu halisi. Watu wengi hawamjui Zari. Hawajui maisha halisi ya Zari. Wengi wanakisia tu katika mitandao. Huwa sijibishani na watu mitandaoni. Nitabishana na watu wangapi? Lakini, katika kipindi changu cha TV ‘Maisha ya Zari’ nadhani wengi watamjua Zari halisi.” Anasema kwa kujiamini.
“Kitakuwa kipindi kizuri sana. Watanzania wajiandae kumjua Zari halisi ni yupi. Nina mambo mengi nyuma ya pazia. Unajua kwamba hapa Afrika Kusini nimewekeza kiasi gani? Unajua Ivan aliacha mali kiasi gani? Haya mambo yapo na nayahitaji kuyaendeleza kwa ajili ya watoto wake. Kuna hadi magari yake ya kifahari ambayo binafsi siyaendeshi. Kuna mtoto wake mmoja atatimiza miaka 17 mwakani atayaendesha. Ataruhusiwa kupata leseni ya kujifunza na ataendesha.”
“Nina mambo mengi ya kufanya. Tuna shule hapa. Tuna kampuni ya ulinzi. Nimeajiri watu 360. Ikifika mwisho wa mwezi nalipa mishahara ya watu. Kwa hiyo nikimuona mtu anajaribu kushindana na mimi mitandaoni huwa namshangaa sana. Wanapoteza muda. Mimi Zari nakunywa sehemu kama hii (Sandton), nafurahia maisha sehemu kama hii. Kwanini ubishane na mtu, ambaye hauwezi kushindana naye wala kukutana naye?” Anahoji Zari.
“Huwa nafanya pia mambo ya kijamii lakini sihitaji kujitangaza sana. Kuelekea Sikukuu ya Idd kule nyumbani Uganda nimetuma pesa ndugu zangu walishe yatima nyumbani. Ni maisha yangu binafsi. Ni Zari ambaye wengi hawamfahamu. Wanataka tukae mitandaoni kutukanana bila ya sababu za msingi.”
“Nahangaika na biashara zangu. Ndio maana utasikia leo Zari yupo Uganda, kesho Kenya, keshokutwa London, halafu baada ya hapo Tanzania na kwi ngineko. Mimi ni Mjasiliamali. Nachukia kuona watu hawaufahamu upande huu wa maisha yangu.”
Huyu ndiye Zari ambaye nilikutana naye Sandton na kuufunua moyo wake. Kwa sasa anaonekana mchangamfu, ambaye anajiandaa kufanya mambo mengi makubwa ambayo anataka watu walazimike kumuangalia yeye kama yeye na sio zaidi kuishi katika kivuli cha uhusiano wake uliovunjika kwa sasa na Diamond Platnumz. Tusubiri.

-mwananchi

Download App Yetu MPYA  >> BOFYA HAPA << Tukutumie Habari na Burudani Zote FASTA Kila Siku !

No comments

TOA MAONI YAKO HAPO CHINI.