Roma 4-2 Liverpool: Jurgen Klopp Asema Mechi ya ligi ya UEFA Ilikuwa 'Wazimu' - BongoSwaggz.Com

Advert

Breaking News

Roma 4-2 Liverpool: Jurgen Klopp Asema Mechi ya ligi ya UEFA Ilikuwa 'Wazimu'

Meneja wa klabu ya Liverpool ya England Jurgen Klopp amesema klabu yake ilicheza kandanda "wazimu" kufanikiwa kufika Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.

Hii ni baada ya kupata ushindi wa jumla wa 7-6 dhidi ya AS Roma ya Italia hata baada ya kushindwa 4-2 kwenye mechi ya marudiano iliyochezewa Italia Jumatano.

Liverpool sasa watakutana na miamba wa Uhispania real Madrid mjini Kiev mnamo 26 Mei kwenye fainali.

Klopp alieleza mechi hiyo kama ya kushangaza lakini akaongeza kwamba: "Ilikuwa kiasi inavutia zaidi - ilivutia zaidi kuliko nilivyotaka kusema kweli."

"Ilikuwa na nusu fainali ya kwanza kwa wengi wa wachezaji kwa hivyo ilikuwa kawaida kwao kuingiwa na wasiwasi."

Liverpool walishinda mechi ya mkondo wa kwanza Anfield 5-2 na Klopp amesisitiza kwamba wanastahiki asilimia 100 kuwa kwenye fainali.

Hata hivyo, amedokeza kwamba walihitaji bahati kiasi kufanikiwa.

"Hauwezi kufanikiwa bila bahati. Tuliihitaji bahati mara moja pekee usiku huu. Real Madrid walihitaji pia kubahatika," aliambia BT Sport baada ya mechi.
Wachezaji wa Liverpool wakisherehekea chumbani baada ya mechi

"Vijana hawa wanastahiki, mtazamo wao, kujituma kwao na kiwango cha soka walichoonyesha - ilikuwa wazimu kusema kweli."

Liverpool tayari wameshinda Kombe la Ulaya mara tano - mara nyingi zaidi kushinda klabu yoyote kutoka England.

Ushindi wao wa karibuni zaidi ulikuwa mwaka 2005 walipotoka nyuma 3-0 kufikia wakati wa mapumziko na kuwalaza AC Milan kwa mikwaju ya penalti.

Liverpool wamekuwa wazuri kiasi gani msimu huu?

Mohamed Salah (10), Roberto Firmino (10) na Sadio Mane (9) sasa ndio wachezaji watatu wa klabu moja waliofunga mabao mengi zaidi kwa pamoja msimu mmoja wa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya - wamewapita Cristiano Ronaldo, Gareth Bale na Karim Benzema wa Real Madrid walioweka rekodi msimu wa 2013-14.

Liverpool wamefunga mabao 20 ugenini Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya msimu huu, ambayo inafikia rekodi ya mabao ya ugenini msimu mmoja ligi hiyo (iliyowekwa na Real Madrid 2013-14).

Liverpool pia wamekuwa klabu ya tatu kufunga mabao 40 msimu mmoja wa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya baada ya Barcelona (45 in 1999-00) na Real Madrid (41 in 2013-14).

Liverpool ndiyo klabu ya kwanza kuwafunga bao Roma kwao nyumbani Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya msimu huu.

Aidha, ndiyo timu pekee iliyofunga mabao matano na zaidi katika mechi nne msimu mmoja Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.

Liverpool ndiyo klabu pekee ambayo ilikuwa haijashindwa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya msimu huu kabla ya mechi ya marudiano iliyochezwa Jumatano Roma (Walikuwa wameshinda 7 na kutoka sare mechi 4)

Liverpool wamefika fainali Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya/Kombe la Ulaya mara ya nane (ya kwanza tangu 2007), mara tatu zaidi ya klabu nyingine yoyote ya England.

Baada ya kufungwa mabao 13 mikondo yote miwili, nusufainali ya Liverpool na AS Roma ndiyo iliyoshuhudia mabao mengi zaidi kufungwa nusufainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya, ambayo imeipita Monaco v Juventus (4-6) mwaka 1998.

'Wachezaji walisemaje?

Nahodha Jordan Henderson (kulia) akisherehekea na Mohamed Salah

Kiungo wa kati James Milner: "Tunajua kukoleza uhondo, si ndio? Hivyo ndivyo mambo yanavyokuwa, tunayoyaona hapa leo.

"Hakuna aliyesema kwamba kufika fainali Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya itakuwa rahisi na tumezishinda timu kubwa njiani hadi tukafika hapa. Muhimu leo ilikuwa kumaliza kazi na sasa tumefika fainali.

"Ni lazima tusherehekee hili lakini si kwa muda mrefu kwani tuna mechi nyingine muhimu wikendi. Ninaweza kujivinjari na kuburudika na Ribena au kitu kingine, pengine!"
Sadio Mane alifunga bao la kwanza dhidi ya Roma na alitawazwa mchezaji bora wa mechi

Beki Andy Robertson: "Ni jambo zuri ajabu ambalo tumeshiriki katika! Tumepitia vikwazo vyote tulivyowekewa. Tutakuwa na siku nzuri sana Kievi - bila kujali matokeo.

"Msimu uliopita tulikuwa tunapigania kunusurika Hull, sasa ni kama tumefika nyumbani. Bila shaka nitafurahia mambo Kievi.

Kiungo wa kati Georginio Wijnaldum: "Itakuwa mechi nzuri sana [dhidi ya Real Madrid]. Iwapo unataka kushinda Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya ni lazima uichape timu yoyote ile. Wana wachezaji wazuri lakini nasi tunao pia."

Nahodha Jordan Henderson: "Huwa hatufanyi mambo kwa ile njia rahisi lakini tulifanya vyema sana. Kwa jumla, tulishughulikia hali yote vyema, ila dakika 10 za mwisho. Ni lazima tukomeshe hilo lakini tunafurahia kufika fainali.

"Tuna mechi nyingine muhimu wikendi dhidi ya Chelsea na kisha kuna Real Madrid fainali. Lazima tufike huko tukiwa tunajiamini."

Download App Yetu MPYA  >> BOFYA HAPA << Tukutumie Habari na Burudani Zote FASTA Kila Siku !

No comments

TOA MAONI YAKO HAPO CHINI.