HII KALI: Alikiba, Abdul Kiba Kufunga Ndoa Siku Moja - BongoSwaggz.Com

Advert

Breaking News

HII KALI: Alikiba, Abdul Kiba Kufunga Ndoa Siku Moja

ULISHAWAHI kutembea barabarani ukiwa umeshika pakti ya ubuyu mtamu? Hakika huwezi kupiga hatua mbili bila kuombwa, iwe na mtoto, kijana au mzee! Basi ubuyu wa motomoto uliotufikia mezani kwetu ni kwamba yule mwanamuziki mkubwa wa Bongo Fleva, Ali Saleh Kiba ‘Alikiba’ na mdogo wake ambaye naye ni staa wa Bongo Fleva, Abdul Kiba wanaounda muunganiko wa Kiba Square, wanatarajia kuvuta jiko kwa pamoja hivi karibuni.

CHANZO CHATIRIRIKA

Chanzo makini kutoka ndani ya familia ya Kiba, kilimwaga ubuyu kuwa, vikao na shamrashamra za hapa na pale vimeanza ndani ya familia hiyo huku vikiwashirikisha watu wa karibu ambao wameamua kufanya harusi ya ndugu hao siku moja.

“Hivi ninavyokuambia vikao vinaendelea vya kimyakimya, ndugu wa karibu tu ndiyo wanahusika.

“Itakuwa ni harusi kubwa kwa sababu ni ndugu wawili wenye majina hapa Bongo na nje ya Bongo pia ndiyo wanaoa, lakini wamependa kufanya kimyakimya kwanza,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:

“Unajua kila mmoja ana mashabiki wengi hivyo siyo shughuli ndogo kama wenyewe wanavyotaka kufanya iwe siri.”

WANAWAKE AMBAO WANATARAJIA KUWAOA

MSAMBAZA ubuyu huyo alinyetisha kuwa, wanamuziki hao wanatarajia kuoa wanawake ambao hawana hata chembe ya ustaa huku kwa upande wa Kiba mkubwa ikifahamika kuwa anamuoa mwanamke kutoka nchi jirani ya Kenya.

“Unajua kwa Kiba kumuoa mrembo huyo wa Mombasa itazima kabisa minon’gono mbalimbali ya kuwa nani ataolewa naye.

“Abdul Kiba yeye mwanamke wake ni wa hapahapa,” kilizidi kudokeza chanzo hicho.

KIBA KUHAMIA KWENYE JUMBA LAKE AKISHAVUTA JIKO

Mtoa habari wetu huyo alizidi kuweka wazi kwamba, hata nyumba ya kifahari ambayo ameijenga Kiba maeneo ya Tabata, Dar alipewa sharti na mama yake mzazi kuwa, hawezi kuingia ndani yake hadi aoe na ndivyo inavyosubiriwa kwani baada ya harusi ndipo atahamia rasmi kwenye mjengo huo.

“Hiyo nyumba ya Tabata inasubiri tu Kiba amalize kufunga ndoa ndipo ahamie kwa sababu tayari ina kila kitu na kilichokuwa kikisubiriwa ni harusi tu,” kilisema chanzo hicho.

HUYU HAPA ABDUL KIBA

Baada ya kunyaka ubuyu huo, kama ilivyo desturi yake, Ijumaa Wikienda lilianza kwa kumsaka Abdul Kiba na kumuuliza kuhusiana na ubuyu huo ambapo alifunguka kama ifuatavyo;

Ijumaa Wikienda: Vipi Abdul, umekuwa kimya sana, ni kwa sababu ya harusi?

Abdul: Harusi ya Ali au?

Ijumaa Wikienda: Si na wewe pia maana ninasikia mnaoa siku moja?

Abdul: Anayeoa ni Ali, mimi sina mpango wa kuoa mwaka huu kabisa.

Ijumaa Wikienda: Ila wanasema mnafanya pamoja na mchumba wako ameshafanyiwa kibao kata, je, ni kweli?

Abdul: Si unajua mambo ya wanawake? Lakini ndoa mimi bado, Ali ndiyo anatarajia kuvuta jiko mwezi ujao (Machi). 


-GPL

Download App Yetu MPYA  >> BOFYA HAPA << Tukutumie Habari na Burudani Zote FASTA Kila Siku !

No comments

TOA MAONI YAKO HAPO CHINI.