Fahamu Jinsi ya Kupata Mtoto wa Kiume, Soma Hapa - BongoSwaggz.Com

Advert

Breaking News

Fahamu Jinsi ya Kupata Mtoto wa Kiume, Soma Hapa

KAMA wewe ni mzazi unayetamani kuwa na watoto wa jinsia uitakayo, bila shaka hii inaweza kuwa habari njema zaidi kwako.
Ni kwamba, kuna njia kadhaa za kitaalamu zinazoweza kutumiwa na wazazi ili kujipatia watoto wanaoweza kujiamulia kuwa wawe wa kiume au wa kike.
Uchunguzi uliohusisha mahojiano na madaktari kadhaa wakiwamo mabingwa wa masuala ya uzazi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, umebaini kuwa sasa wazazi wanaweza kufanikisha ndoto ya kupata watoto wa kiume au wa kike kadri watakavyo kwa njia rahisi inayotoa matokeo chanya kwa asilimia 80 au nyingine ya kitaalamu zaidi inayopatikana pia nchini na ambayo matokeo yake huwa na uhakika wa takribani asilimia 100.
Kupitia mahojiano hayo na wataalamu, Imebainika kuwa karibu wote humtanguliza Mwenyezi Mungu katika kufanikisha jambo hilo.
Akizungumza katika mahojiano maalum yaliyofanyika Alhamisi, Daktari Bingwa wa Wanawake katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Living Colman, alisema jambo hilo linawezekana lakini kuna mambo muhimu ya kuzingatia kabla wazazi kupata mtoto wa jinsia waitakayo.
Alisema wahusika ni lazima wawe na afya njema na pia mbegu kutoka kwa mwanaume lazima ziwe na ubora unaotakiwa katika kufanikisha utungaji wa mimba.
Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, Tanzania ina watu milioni 45, huku wanawake wakiwa milioni 23, sawa na asilimia 51.
NJIA KUPATA MTOTO WA KIUME, KIKE
Wakizungumza, baadhi ya madaktari waliitaja njia ya upandikizaji wa mbegu kuwa ndiyo kubwa na ya uhakika zaidi kufanikisha utungaji wa mimba ya mtoto wa jinsia waitakayo wazazi.
Hata hivyo, Dk. Colman aliiambia gazeti hili kuwa mbali na njia hiyo inayohusisha matumizi ya maabara, ipo njia nyingine rahisi inayotokana na ufuatiliaji makini wa kalenda ya mzunguko wa hedhi wa mama.
“Hii ni rahisi zaidi na haihusishi upandikizaji wa mbegu kwenye maabara… hata hivyo, njia hii inahitaji wahusika kuwa makini zaidi katika kufuatilia mzunguko wa hedhi wa mama kwa sababu kinyume chake matokeo huwa hafifu,” alisema Dk. Colman.
Akieleza zaidi, Dk. Colman alisema wengi hujaribu kufuata njia hiyo ya kalenda na kupata matokeo hasi kwa sababu ya kutozingatia maelekezo, lakini ukweli ni kwamba yenyewe hutoa matokeo ya uhakika kwa asilimia 80.
“Kati ya watu 10 wanaokuja kwangu na kuomba ushauri wa namna ya kupata watoto wa jinsi waitakayo, nane wamefanikiwa… kwa hiyo hii inawezekana kabisa,” alisema Dk. Colman.
UFAFANUZI NJIA YA KALENDA
Wakati baadhi ya madaktari wakitilia shaka njia ya kalenda, Dk. Colman anasisitiza kuwa huleta mafanikio chanya kwa kiasi kikubwa na kwamba, lililo muhimu ni kwa wazazi kuwa na utimamu wa kiafya na kubwa zaidi ni kuzingatia muda sahihi wa kushiriki tendo la ndoa kwa nia ya kupata mtoto.
Akifafanua, Dk. Colman alisema daima, mwanamke huzalisha mbegu aina moja zinazotambulika kama ‘XX’ na hizo huendeleza ukike. Kwa wanaume, mbegu zinazozalishwa huwa ni za aina mbili ambazo ni ‘X’ (kike) na ‘Y’ (kiume).
Alisema kuwa mbegu yoyote ya mwanamke (X) ikichavushwa na mbegu ‘X’ ya mwanaume hutengeneza muunganiko wa ‘XX’ ambao mwishowe huwa ni kutungwa kwa mimba ya mtoto wa kike. Hata hivyo, inapotokea mbegu ya mwanamke ikakutana na mbegu ‘Y’ hutokea muunganiko wa ‘XY’ ambao mwishowe huwa ni mimba ya mtoto wa kiume.
Akieleza zaidi, Dk. Colman alisema kuwa sifa ya mbegu ‘X’ huwa ni uimara wake kulinganisha na mbegu ‘Y’, lakini pia huwa na mwendokasi mdogo kulinganisha na mbegu ‘Y’ ambazo zenyewe huwa hazidumu muda mrefu kabla ya kuharibika kwa vile siyo imara kulinganisha na ‘X’, na zina mwendokasi mkubwa zaidi.
“Mbegu X ipo imara lakini inapotoka huenda taratibu wakati mbegu Y ni dhaifu, lakini mwendo wake huwa ni wa kasi zaidi,” alisema.
Kwa sababu hiyo, Dk. Colman alisema wazazi wanapaswa kuzingatia kalenda ya mzunguko wa hedhi ili kufanikisha mimba ya mtoto wa kiume au wa kike kulinga na na vile watakavyo.
“Ni lazima ujue mzunguko wa mwanamke husika ni wa aina gani… kwa maana kuna mizunguko ya wastani wa siku 28 ambayo hii yai lake hutoka siku ya 14, kuna mzunguko mfupi wa siku 21 na yai hutoka siku ya 10 na pia wale wa mzunguko mrefu wa siku 36 ambao yai hutoka katika siku ya 18,” alisema.
"Kwa kawaida, yai hutoka katikati ya mzunguko wa mwanamke kulingana na mzunguko wake. Hivyo, mbali ya kujua hilo la mzunguko, ni lazima wazazi watambue tabia za mbegu X inayosafiri taratibu na Y inayosafiri haraka… hilo ni muhimu kwa sababu ndilo husaidia katika kufanikisha ndoto ya kuchagua jinsia ya mtoto," alisema.
Aliongeza kuwa wahusika wakishiriki tendo la ndoa siku mbili au tatu karibu na yai la mama kutoka, maana yake kutakuwa na uwezekano mkubwa wa kutungwa kwa mimba ya mtoto wa kiume kwa vile kutokana na tabia ya mbegu Y ya kusafiri kwa kasi, maana yake ndiyo itakayotangulia na hivyo kukutwa na mbegu ya mama wakati nyingine ya X ikiwa imeachwa kwa vile kasi yake ni ndogo.
Alisema kwa sababu hiyo, wazazi wanaoota kupata mtoto wa wa kiume watalazimika kushiriki tendo la ndoa wakati zikiwa zimebaki siku mbili au tatu kabla ya yai la mama kutoka.
Aidha, Dk. Colman alisema ikiwa wazazi watakuwa na ndoto ya kupata mtoto wa kike, watalazimika kushiriki tendo la ndoa siku nyingi, kati ya 9, 10 au 11 kabla ya siku inayotarajiwa kuwapo kwa yai la mama katika mzunguko wake.
Alisema hilo ni muhimu kuzingatiwa kwa sababu kutokana na tabia ya mbegu X (kike), maana yake mwendo wake utakuwa wa taratibu na itadumu kwa siku hizo nyingi kabla ya kukutwa na kukutana na mbegu itokayo kwa mama huku mbegu Y ikiwa tayari imeshaharibika kutokana na kutangulia kwake mbele haraka na kukosa uimara wa kusubiria siku zote hizo.
“Mkishiriki tendo la ndoa mapema kidogo, kama siku mbili au moja hivi karibu na yai kutoka, mtapata mtoto wa kiume. Lakini ikiwa ni siku nyingi kabla ya hapo kuna uwezekano mkubwa wa kupata mtoto wa kike,” alisema Dk. Colman kabla ya kutahadharisha kwa kuongeza:
“Ila hizi zote siyo kanuni za kudumu maana mwili wa binadamu hubadilika… lazima hili lifanyike kwa kuzingatia mzunguko wa mwanamke na hiyo ni kwa mujibu wa matokeo ya tafiti.”
Aidha, Dk. Colman alisisitiza kuwa msingi wa mafanikio ya mpango huo wa kuchagua jinsia ya mtoto kwa kuratibu mzunguko wa hedhi ya mama ni kujua kwa usahihi siku za mzunguko huo.
“Kikubwa ni mwanaume na mwanamke kujua yai linatoka lini ili mbegu X au Y zikutane na yai la mwanamke na kufanikisha utungwaji wa mimba ,” alisema Dk. Colman.
Aliongeza kuwa, endapo kuna wazazi wanapenda kuwa na watoto wa jinsia tofauti, ni vyema wakazingatia njia hiyo isiyogharimu chochote ya kuzingatia vyema mzunguko wa hedhi wa mwanamke kama ni wa kawaida, mrefu au mfupi.
Alisema eneo hilo ndilo huwashinda wengi na kupata matokeo tofauti na yale wanayoyatarajia.
“Hapa wengi huchanganya sana. Unakuta mwanamke mzunguko wake ni wa siku 28 na hivyo yai hutoka siku ya 14, lakini wawili hao wanatumia kanuni nyingine ya mzunguko mfupi wa siku 21 ambayo yai hutoka siku ya 10.
Ni lazima pia kuzingatia muda wa kushiriki tendo la ndoa kulingana na tabia nilizozitaja za X na Y,” alisema Dk. Colman.
“Hadi sasa, katika watu 10 walionifuata na kuniomba ushauri wa kupata watoto wa jinsia waitakayo, nane wamefanikiwa (asilimia 80). Kwa hiyo utaona kwamba jambo hilo linawezekana, ila muhimu ni kuzingatia masuala hayo ya mzunguko wa mama na siku ya kushiriki tendo la ndoa,” alisema.
NJIA YA UPANDIKIZAJI
Mbali na njia ya kuzingatia mzunguko wa mama kabla ya kushiriki tendo la ndoa ambayo haileti mafanikio kwa asilimia 100, Dk. Colman aliitaja njia nyingine inayotoa fursa kwa wazazi kuchagua jinsia ya mtoto kuwa ni ile ya upandikizaji mbegu kwa mama kuwa ndiyo ya uhakika zaidi katika kuchagua jinsia ya mtoto.
Hata hivyo, Dk. Colman alisema teknolojia hiyo ya upandikizaji ni ghali na kwa hapa Tanzania bado ni ngeni na haipo katika hospitali za Serikali.
“Upandikizaji mbegu unaanzia kwa kutolewa mbegu mwanaume na baadaye kupelekwa maabara. Huko hupimwa magonjwa yote ili kujua ubora wake. Pia ni huko maabara ndipo wazazi wanapoweza kujua jinsia ya mtoto wao kwa asilimia 100. Na hii ndiyo njia sahihi na ya uhakika zaidi,” alisema Dk. Colman.
Aliongeza kuwa katika siku zijazo, anaamini kuna wakati hospitali yao (Muhimbili) itatimiza lengo la kuanzisha Kitengo Maalum cha Matatizo ya Ujauzito na Uzazi ambako humo, watakuwa na fursa ya kuwasaidia watu wanaohitaji huduma ya upandikizaji wa mbegu kwa ajili ya kupata watoto.
KLINIKI YA UPANDIKIZAJI DAR
Katika uchunguzi wake, mwandishi alipata bahati ya kutembelea kituo cha tiba kilichoanzishwa miaka ya hivi karibuni katika maeneo ya Mikocheni jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kushughulikia matatizo ya uzazi huku pia kikiwa na teknolojia ya kupandikiza mbegu kiitwacho Dar IVF and Fertilizing Clinic.
Mkurugenzi wa Tiba wa kituo hicho, Dk. Tamale Sali, alizungumzia pia uwezekano wa wazazi kupata watoto wa jinsia watakayo kwa kutumia teknolojia ya upandikizaji na kuleta matokeo sahihi ya asilimia 100.
“Tafiti nyingi zinaonyesha kuwa hii njia ya kuchagua jinsia ya mtoto kwa mzunguko wa hedhi hutoa matokeo ya asilimia 50 kwa 50. Siyo ya uhakika sana kwa sababu wazazi wanaweza wanaweza kufanikiwa au wasifanikiwe.
Lakini ya upandikizaji maabara ina uhakika zaidi katika kupata mtoto wa jinsia wanayoitaka wazazi,” alisema Dk. Sali.
Akieleza zaidi, Dk. Sali alisema kinachoweza kufanyika kwa wale wanaotaka kuwa na watoto wa kiume au wa kike kadri watakavyo ni kuchukuliwa kwa mbegu za mwanaume, kupelekwa maabara na huko ndiko uamuzi kuhusu jinsia ya mtoto unaweza kutolewa na wahusika.
Aidha, Dk. Sali aliongeza kuwa mbali na uamuzi kuhusu jinsia ya mtoto, wazazi hupata fursa pia ya kupata mtoto asiyesumbuliwa na maradhi kama ya kisukari na moyo.
“Mbali ya kupimwa jinsia ya mtoto, mbegu ya baba hupimwa pia magonjwa mengine kama ya moyo na kisukari… kama itabainika kuwa mbegu ina tatizo, inaachwa na kuchukuliwa mbegu nyingine,” alisema.
Dk. Sali alisema kuwa hadi sasa, tangu waanze kutoa huduma zao nchini, tayari wameshasaidia wazazi tofauti 15 kupata watoto wa jinsia waitakayo kwa njia ya upandikizaji huku wastani wa watoto wanaozaliwa nchini Uganda kwa mwaka kupitia njia hiyo katika kliniki yao iliyopo nchini humo ni 30.
Alisema wanaopaswa kutumia njia ya upandikizaji katika kupata watoto ni wanawake ambao mirija yao ya uzazi imeziba, wale walio na utasa na baadhi ya wagojwa wenye uvimbe kwenye ‘ovari’, vivimbe vya vimeleo kuzunguka mfuko wa uzazi, wanawake waliomaliza hedhi na bado wanahitaji mchango wa mayai, waliotolewa mfuko wa uzazi lakini ovari zao zimebaki na sababu nyingine za kijamii ikiwamo mume kusafiri kwenda masomoni au vitani.
Alisema kwa kawaida, wao hutoa matibabu kwa njia ya upandikizaji pale tu inapowalazimu wanandoa kufanya hivyo ikiwa ni njia ya mwisho baada ya njia nyingine zote za kupata mtoto kugonga mwamba.
MSIMAMO WA SERIKALI KUHUSU JINSIA ZA WATOTO
Baadhi ya watu hutamani kuwa na mchanganyiko wa jinsia katika orodha ya watoto wao na hivyo huwa tayari kufuata njia mbalimbali ili kuwapata watoto wa jinsia waitakayo ili kukidhi matakwa yao.
Hata hivyo, imebainika kuwa baadhi ya njia haziruhusiwi nchini ikiwamo ile ya kukatisha uhai wa mimba ya mtoto wa jinsia wasiyoitaka wazazi wakati wa kutungwa kwake.
Mkurugenzi wa Uhakiki wa Ubora wa Huduma katika Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Mohamed Mohamed, alisema ni kosa kisheria kwa mama kutoa mimba baada ya kujua jinsia ya mtoto anayetarajia kumzaa.
Kuhusu upandikizaji alisema sheria inatambua wale wenye matatizo ya uzazi, wenye umri mkubwa na ukomo wa hedhi kuwa hawakatazwi kupandikiza lakini siyo wanandoa wenye afya njema na uwezo wa kupata watoto kwa njia ya kawaida.

Download App Yetu MPYA  >> BOFYA HAPA << Tukutumie Habari na Burudani Zote FASTA Kila Siku !

No comments

TOA MAONI YAKO HAPO CHINI.