Wazazi wasimulia walivyopokea msiba - BongoSwaggz.Com

Advert

Breaking News

Wazazi wasimulia walivyopokea msiba

TAIFA liko katika maombolezo makubwa ya msiba wa wanafunzi 33, walimu wawili na dereva wa Shule ya Msingi ya Mchepuo wa Kiingereza ya St Lucky Vincent, ambao walikufa baada ya gari lao kutumbukia kwenye korongo la Mto Marera, Kata ya Rhotia wilayani Karatu mkoani Arusha juzi asubuhi huku baadhi ya wazazi wakisimulia jinsi waliovyoupokea msiba huu mzito.

Tangu baada ya taarifa za ajali za msiba huo kusambaa katika mitandao ya kijamii, siku nzima ya juzi ikawa ya majonzi makubwa ambayo yameendelea kwa siku nyingine ya jana na zaidi leo wakati itakapofanyika ibada maalumu kwenye Uwanja wa Michezo wa Shehe Amri Abeid Kaluta, katikati ya Jiji la Arusha. Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, alitarajiwa kutua jana jijini humo na leo anatarajiwa kuongoza mamia ya wakazi wa Arusha na mikoa ya jirani watakaohudhuria ibada maalumu itakayofanyika uwanjani hapo kwa ajili ya heshima ya watu hao 36 waliopoteza maisha wakiwa safarini kwenda katika mitihani ya ujirani mwema mjini Karatu.

Mbali ya Makamu wa Rais, viongozi wengine wa serikali watakaoshiriki ibada hiyo ni Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana.

GAMBO ATOA RATIBA Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo aliwaambia wanahabari jana kuwa viongozi hao wamethibitisha kushiriki ibada hiyo itakayoanza saa mbili asubuhi. Gambo alisema miili yote ya wanafunzi waliokufa katika ajali hiyo itakuwepo kwenye uwanja huo na kufanyiwa ibada kabla ya kuchukuliwa na ndugu, jamaa kwa ajili ya kwenda katika maziko mahali watakapokuwa wamekuchagua.

Aliwataka Watanzania waliopo jijini Arusha na nje ya Arusha kuja kwa wingi katika ibada hiyo yenye simanzi kubwa kwa Watanzania wote kote nchini. Wanafunzi hao walipata ajali katika eneo la Rhotia na gari aina ya Mitsubishi Rosa lenye namba za usajili T871BYS lililokuwa likitoka jijini Arusha kwenda katika Mji wa Karatu kupata ajali ya kutumbukia mtoni na kusababisha vifo hivyo. Wanafunzi hao waliondoka jijini Arusha saa mbili asubuhi kuwahi mtihani huo wa majaribio wa kirafiki na wenzao wa Shule ya Msingi ya Tumaini Junior ya Karatu.

MAJINA YA WALIOKUFA Majina ya wanafunzi walikufa wametajwa kuwa ni Aisha Said, Anold Alex, Gladness Goodluck, Junior Mwashuy, Praise Ronald, Witness Moses na Heavenlight Mcharo. Wengine ni Eliapenda Eliudi, Rukia Halfan, Justine Alex, Rehema Msuya, Irene Kishari, Prisca Charles, Ian Tarimo, Shedrak Bikhet, Sabrina Saidi, Rachel Gidion, Irene Moses, Hagai Lucas.

Pia wamo Rehema Eliwadi, Rebeca Daudi, Dismas Kessy, Innocent Papian (mwalimu), Oumuh Rashid, Gema Gerald, Grayson Masawe, Julius Bonge Mollel (mwalimu), Joel Lucas, Naomi Hosea, Ruth Ndemno, Saada Ally, Neema Martin, Witness Philemon na Musa Khamis. Aidha, kwa mujibu wa mtu wa mtumishi wa chumba cha maiti Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru, ambaye hakupenda kutaja jina lake, baadhi ya miili ya watoto hao imehamishiwa Hospitali ya Selian kwa sababu mochwari ya Mount Meru ilikuwa imejaa, hivyo maiti zilizohamishiwa huko ni saba ambazo ni Neema Martin, Oumuh Rashid, Gema Mchome, Irene Moses, Rebeka Daudi, Hagai Lucas na Rachel Gidion.

Wazazi na walezi walikusanyika tangu asubuhi ya jana kwenye Hospitali ya Mount Meru kwa ajili ya kuwaona watoto hao huku wakisoma majina yaliyobandikwa ili kujua kama wapo hospitali hiyo au Hospitali ya Selian. WAZAZI WASIMULIA WALIVYOPOKEA MSIBA Katika hatua nyingine, badhi ya wazazi wameelezea jinsi walivyopokea msiba kwa huzuni na wengine wakisema ni jambo la kushukuru kwa yote kwani mapenzi ya Mungu yametimizwa.

Wakizungumza katika maeneo tofauti ya Kwamrombo katika eneo la Baa Mpya na Mtaa wa Mlimani Kata ya Terrat, baadhi ya wazazi hao walioondokewa na watoto wao, walisema inaumiza kwani baadhi ya watoto walikuwa wakikaa shuleni wakiwa darasa la saba huku wengine wakitokea nyumbani kwenda ziara ya kimasomo Karatu. Mzazi wa marehemu Irene Moses (13) ambaye ni Mosses Kivuyo anayefanya kazi Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga ambaye sasa yupo masomoni Chuo cha Ufundi Arusha, alisema mtoto wake Irene alikwenda Karatu na wenzake, lakini ghafla alisikia taarifa kuwa watoto hao wamepata ajali.

Alisema hakujua kama mwanawe ni miongoni mwa waliokufa, lakini alijipa moyo na kisha kuanza safari ya kutoka Arusha kwenda Rothia kwa ajili ya kuona watoto hao akiwemo mwanawe Irene na alipokuwa njiani, alipigiwa simu na wauguzi wakisema mtoto wake anataka kufanyiwa upasuaji, lakini wameamua kwanza wampigie simu. ASHUHUDIA MWANAWE AKIKATA ROHO Alisema aliwajibu wauguzi hao kwamba yuko njiani anakwenda na alipokaribia eneo la tukio hakumwona binti yake hivyo akaenda hospitali sababu alipigiwa simu kwani mtoto wake ndiye alisema apigiwe simu akiwa majeruhi “ndipo niliondoka kwenda kumuona Hospitali ya Karatu kumuona ndipo nilipofika tu mtoto wangu namuona akifa.” “Ukweli nimeumia kama mzazi.

Huyu ni mtoto wangu wa kwanza kati ya watoto watatu sasa huu msiba ni mzito sana kwetu wazazi tulioondokewa na watoto... inauma jamani, lakini haya ni mapenzi ya Mungu nashukuru kwa hili. Lakini nimeumia nafika tu hospitali mtoto anakufa jamani Irene wangu,” alieleza Moses. Naye mzazi wa marehemu Oulu Rashid, Msagaya Kimea alisema taarifa za mtoto wake kufa alizipata kupitia mitandao ya kijamii akiwa nyumbani kwake Kwamrombo, alipomuona mkewe akilia.

Alimwacha nyumbani kisha yeye kutoka hadi barabarani kupiga simu kwa Meneja wa Shule ya Lucky Vicent ili kuthibitisha taarifa hizo na meneja huyo alimweleza juu ya tukio hilo kisha alikwenda Hospitali ya Mount Meru kwa ajili ya kuona miili ya watoto hao. AONA JINA KUPITIA MITANDAO Alisema alikaa hospitali kwa muda mrefu kusubiri watoto wao waletwe, lakini ghafla aliona kupitia mitandao ya kijamii majina ya watoto waliokufa likiwamo jina la mwanawe.

“Nilishtuka nikajipa moyo maana sikujua kama mwanangu huo ndio ulikuwa mwisho wake maana alihamia shuleni kukaa huko, yaani nimeumia lakini ni jambo la kushukuru Mungu kwa kila jambo “. Awali shuleni hapo wakizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Lucky Vicent, Severine Laswai, alisema ajali hiyo ni huzuni kubwa kwa wananchi, walimu ndugu, jamaa na marafiki na jumla ya wanafunzi waliopata ajali hiyo ni 33 wakiume wakiwa ni 13 na wakike 20, walimu wawili na dereva mmoja Alisisitiza kuwa huu msiba ni wa kitaifa hivyo hawezi kuongelea zaidi juu ya tukio hilo kwani hivi sasa wanaandaa taarifa zaidi, lakini alisisitiza kuwa hilo ni pigo kubwa kwao.

DEREVA WA SHULE Naye Mkuu wa Shule hiyo, Ephraim Jackson, alisema nipo katika wakati ngumu sana. “Kwa kweli siwezi kuongelea suala hili kwa undani sana, lakini nataka kuwaambia kuwa dereva aliyekufa ni dereva wa shule yangu ni mwajiriwa hapa shuleni na hilo gari ni gari la shuleni kwangu wala sijakodisha,” alibainisha. “Yanasemwa mengi, lakini huyu dereva ambaye ni marehemu ni dereva wangu na hilo gari lililopata ajali ni gari la shule.

Huu ni msiba mzito na unaniumiza sana,” alisema Jackson. Kwa mujibu wa wafanyakazi shuleni hapo, wanadai kuwa dereva huyo ana mwaka mmoja kazini na alikuwa akiendesha gari dogo la shule na hiyo ilikuwa ni safari yake ya kwanza kwenda mbali na kuendesha basi kubwa. Aidha, baada ya ajali hiyo, wanafunzi wengine waliokuwa katika mabasi mawili kati ya matatu yaliyokuwa katika msafara huo, walirejea shuleni kwa kutumia mabasi yao ya shule kisha kuruhiswa kurejea nyumbani na wazazi wao waliokuwepo shuleni hapo.

LA SABA WALIKUWA 106 Alisema watoto walikwenda kwenye ziara ya kimasomo na ni utaratibu wa shule kwenda kushindana na shule zingine huku akisema shule hiyo ya Lucky Vicent English Medium ilianza mwaka 2006, na wanafunzi wanaotarajia kumaliza darasa la saba wakiwa ni 106, lakini sasa watabaki 73 baada ya wenzao hao 33 kufariki juzi. “Siwezi kusema zaidi ya haya kwa kweli maana nimeumia juu ya watoto hawa maana tumewafundisha wengine tangu shule za awali na hadi sasa wamekuwa wakubwa ndiyo wanakufa.

Ukweli sisi tumepata pigo kama walimu watoto hawa tumewazoea na leo hii wamekufa kweli kama walimu tumepata ganzi kwenye miili yetu, sijui tutafundishaje maana hii picha haitatutoka mapema,” alisema Jackson. Kwa upande wake, mwalimu Julius huku akilia alisema, “Hii ni huzuni fikiria watoto mnawafundisha leo hii unaona kabisa mwanga wa maisha yao wengine wakiniona walikuwa wakisema mwalimu nataka kuwa daktari, mwingine nesi, na wengine walitamka kazi zao, leo hii ndoto zao zimezimika ghafla, kweli huu msiba ni mgumu.

“Siwezi kusema moyoni juu ya tukio hili jinsi nilivyoumia, lakini najiuliza watoto wengine wakirudi shuleni kuendelea na masomo hali itakuwaje, marafiki zao hapa shuleni je watasemaje, tutawajibu nini watoto hawa yani naanza kuandaa majibu ya kujibu watoto hawa ambao ni wadadisi wa mambo.” MEYA: KILA MTAA UNALIA Awali Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro, alisema msiba huo ni mzito kwani kila mtaa watu wanalia. Naye Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, akitoa pole shuleni hapo, alisema amehuzunika juu ya msiba huo kwani umezima ndoto za watoto hao katika kupata elimu na kusisitiza kuwa huo ni msiba mbaya na kuna mambo ya kujifunza juu ya msiba huo ikiwemo masuala ya kurekebisha, hivyo mengine atayaongela bungeni.

“Poleni sana wazazi, walezi, ndugu jamaa na marafiki wote waliokumbwa na msiba huu mzito, kuna mambo mengi ya kujifunza katika msiba huu, lakini nawapa pole wote maana huu msiba ni mbaya sana,” alieleza Lema. SERIKALI KUGHARIMIA SANDA, MAJENEZA Serikali itagharamia sanda na majeneza kwa ajili ya wanafunzi waliopoteza maisha mapema juzi kwenye ajali iliyokuwa ikihusisha safari ya kimasomo.

Akitoa taarifa hiyo jana, Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro, alisema taarifa za awali zinaonesha kuwa tayari serikali imekwishalipia gharama za majeneza na sanda ya kuhifadhia miili ya marehemu ambao leo wanatarajiwa kufanyiwa ibada kwenye Uwanja wa Shehe Amri Abeid Kaluta. Lazaro alisema viongozi mbalimbali wakiwemo mawaziri pamoja na wabunge walikusanyika katika eneo la shule jana kwa ajili ya vikao vya kuandaa ibada hiyo.

Download App Yetu MPYA  >> BOFYA HAPA << Tukutumie Habari na Burudani Zote FASTA Kila Siku !

No comments

TOA MAONI YAKO HAPO CHINI.