Uchinjaji punda kwa kitoweo marufuku - BongoSwaggz.Com

Advert

Breaking News

Uchinjaji punda kwa kitoweo marufuku

KUANZIA Julai Mosi mwaka huu, Serikali imetangaza kusitisha uchinjaji wa punda nchini ili kukabiliana na changamoto ya upungufu au kumalizika kwa wanyama hao kutokana na kasi ya uchinjaji wake inayoendelea.

Pamoja na hayo, serikali hiyo imebainisha kuwa kutokana na ukame uliokumba nchi mapema mwaka huu, umesababisha vifo vya mifugo takribani 132,329 katika mikoa tisa nchini.

Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dk Charles Tizeba, aliyasema hayo mjini Dodoma jana wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2017/18.

Alisema kwa sasa jumla ya punda 500,000 ndio wanakaodariwa kuwepo lakini kasi ya uchinjaji wake ni kubwa na hivyo kuwepo kwa tishio la wanyama hao kutoweka. Alisema baada ya zuio hilo, viwanda na waagizaji wa nyama ya punda, watatakiwa kuachana kabisa na biashara hiyo ya nyama ya punda na badala yake waelekeze nguvu zao kwenye wanyama wengine waliopo nchini.

Akizungumzia tatizo la ukame nchini, alisema ukame huo ulisababisha vifo vya ng’ombe 102,987, mbuzi 14,881, kondoo 13,815 na punda 646 huku mkoa wa Manyara ukiongoza kwa kuwa na vifo vingi vya wanyama hao.

Alisema mkoa wa Manyara ndiyo uliathirika zaidi kwa kupoteza ng’ombe 48,460, mbuzi 13,967, kondoo 12,773 na punda 646 na ndio mkoa pekee uliokuwa na vifo vya punda kutokana na tatizo hilo la ukame.

Alitaja mikoa mingine iliyoathiriwa na ukame huo na kuua wanyama kuwa ni Morogoro ng’ombe 22,939, mbuzi 49 na kondoo 604 kwa upande wa Dodoma ng’ombe 1,041, mbuzi 51 na kondoo 43 na Mara ng’ombe 8,263, Mbuzi 264 na Kondoo 395.

Mikoa mingine ni Pwani ng’ombe 8,256 na mbuzi 475, Shinyanga ng’ombe 5,855 na mbuzi 75, Kagera ng’ombe 7,802, Singida ng’ombe 191 na Arusha ng’ombe 189. Akizungumzia mwenendo wa ulaji wa nyama na maziwa nchini, Dk Tizeba alisema kwa sasa ulaji wa nyama na maziwa kwa watanzania uko chini kwa wastani wa kilo 15l za nyama, lita 47 za maziwa na mayai 106 kwa mtu kwa mwaka.

Alifafanua kuwa kwa mujibu wa viwango vya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) vya mwaka 2011, vinataka mtu ale kilo 50 za nyama, lita 200 za maziwa na mayai 300 kwa mwaka.

Pamoja na hayo, alifafanua kuwa kwa upande wa maziwa, uzalishaji wake umepungua kwa kipindi cha mwaka huu, kwa asilimia 2.3 kutoka lita bilioni 2.14 mwaka 2015/16 hadi lita bilioni 2.09.

Naye Msemaji wa Kambi ya Upinzani bungeni wakati akitoa maoni ya kambi huyo kuhusu bajeti hiyo, Cecilia Pareso, alisema tatizo la ukame limesababisha maafa makubwa kwa wafugaji kwenye maeneo mengi nchini.

Alisema kambi hiyo, ilipata taarifa kamili kutoka kwa wafugaji kuwa wamepoteza mifugo yao hali iliyosababisha wafugaji wengine kufikia hatua ya kujia kutokana na hasara waliyopata.

Download App Yetu MPYA  >> BOFYA HAPA << Tukutumie Habari na Burudani Zote FASTA Kila Siku !

No comments

TOA MAONI YAKO HAPO CHINI.