Kessy afurahia ubingwa huku akimuacha Manara akisubiria pointi za mezani kutoka FIFA - BongoSwaggz.Com

Advert

Breaking News

Kessy afurahia ubingwa huku akimuacha Manara akisubiria pointi za mezani kutoka FIFA

LICHA ya kuwa na msimu uliombatana na ‘misukosuko’ mingi iliyoambatana na ‘kejeli’, mlinzi wa  kulia wa Yanga SC, Hassan Ramadhani Kessy anaweza kutajwa sehemu ya wachezaji walioisaidia sana klabu yake kushinda ubingwa wa tatu mfululizo wa ligi kuu.

Kessy alisaini kuichezea Yanga kabla ya mkataba wake na Simba SC jambo lililoleta mzozo mkubwa msimu huu kiasi cha Yanga kulazimika kukubali kuilipa Simba kiasi cha milioni 50 kama fidia ya kumsaini mlinzi huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar FC.

Kabla ya kuanza kwa msimu wa ligi kuu mwezi Agosti, 2016, Kessy alimudu kucheza michezo miwili kati ya Sita ya Caf Confederation Cup hatua ya makundi. Aliichezea Yanga walipocheza dhidi ya TP Mazembe kisha MO Bejaia na hiyo ilikuwa ni michezo yake ya kwanza ya Kimataifa ngazi ya klabu.

Uwepo wa Juma Abdul katika beki namba mbili ulikuwa kikwazo kikubwa kwa Kessy kuingia katika kikosi cha kwanza mwanzoni mwa msimu huu, sakata la uhamisho wake lilimfanya kuwa mbali na kikosi cha kwanza kwa sababu hata pale alipokosekana Juma Abdul, Mnyarwanda,Mbuyu Twite alikuwa akiziba nafasi yake.

Ikumbukwe katika mchezo wa Ngao ya Jamii ambao ni mahususi kwa kufungua msimu, Kessy alipoteza mkwaju wa penati na kusababisha Yanga kuangusha kikombe cha kwanza msimu huu baada ya kulazwa kwa changamoto ya mikwaju ya penati dhidi ya Azam FC mwezi Agosti, 2016.

Mkufunzi raia wa Holland, Hans van der Pluijm ndiye aliyependekeza usajili wa Kessy kutoka Simba licha ya kuonekana akimtumia kama ‘kiraka wa muda’ tu, ‘babu’ Hans aliamini utafika wakati wa mlinzi huyo kucheza.

Mchezo wake wa ligi kuu akiwa na jezi ya Yanga uliambatana na kichapo cha 2-1 kutoka kwa Mbeya City FC katika uwanja wa Sokoine, Mbeya lakini alinza kupata ushindi wa kwanza akiichezea Yanga wakati kikosi hicho chini ya Hans kilipoifunga Toto Africans 2-0 jijini Mwanza kisha Kagera Sugar FC wakati Yanga iliposhinda ushindi mkubwa zaidi wa msimu-upande wao 6-2 katika dimba la Kaitaba, Bukoba.

Kabla ya mchezo wa kukamilisha msimu dhidi ya Mbao FC, Kessy ameshaichezea Yanga michezo 11 ya ligi kuu, mitatu ya FA Cup na mmoja wa ligi ya mabingwa Afrika.

“Namshukuru Mungu kwa kila jambo, sikuwahi kukata tamaa na nilijitahidi kupambana kila siku ili kuhakikisha nakuwa bora. Kikubwa napenda kuwashukuru wachezaji wenzangu, benchi la ufundi, viongozi, wanachama na mashabiki ambao walinisapoti na kuiunga mkono timu yao,” anasema mlinzi huyo mwenyeji wa Morogoro nilipofanya mahojiano naye.

Nakumbuka mara baada ya Simba kuifunga Yanga 2-1 na kutanua pengo la pointi hadi kufikia tano mwezi Februari, ofisa habari wa Simba, Haji Manara alikuwa kinara wa kuwaongoza wana Simba kumdhihaki Kessy ambaye alikuwa akisotea benchi.

Haji na mashabiki wa klabu yake walimchukulia Kessy ‘mwenye bahati mbaya’ kwani waliamini alipishana na ubingwa huku akikosa nafasi ya kucheza katika michezo yote mitatu ambayo Simba ilikutana na Yanga msimu huu (michezo miwili ya ligi kuu na mmoja wa Mapinduzi Cup 2017)

Miezi isiyozidi mitatu baadae Kessy anashinda taji lake la kwanza la VPL ndani ya misimu yake mitano tangu alipoanza kuichezea Mtibwa Sugar mwaka 2012.

“Kejeli zote kwangu nilichukulia kama changamoto tu. Nilisubiri nafasi na ilipotokea nilijitahidi kuisaidia timu yangu,” anasema Kessy ambaye ameitwa katika kikosi cha timu.

Siku zote ambazo nilipata nafasi ya kubadilishana mawazo na Kessy nilimsisitiza nafasi yake ipo, utafika wakati na huu ni wakati ambao anaingia katika kumbukumbu ya mashujaa wa Yanga akiwa amechezea michezo ya kutosha.

Kessy ameshinda VPL na kumuacha Manara na Simba yake wakisubiri pointi mezani kutoka FIFA ili wajaribu kushinda ubingwa wao wa kwanza wa VPL tangu msimu wa 2011/2012 walipochukua taji hilo kwa mara ya mwisho.

Download App Yetu MPYA  >> BOFYA HAPA << Tukutumie Habari na Burudani Zote FASTA Kila Siku !

No comments

TOA MAONI YAKO HAPO CHINI.