Yanga Yamzuia Msuva Kumzungumzia Fakhi - BongoSwaggz.Com

Advert

Breaking News

Yanga Yamzuia Msuva Kumzungumzia Fakhi

Mshambuliaji wa Yanga, Simon Msuva.

UONGOZI wa Yanga kupitia kwa Makamu Mwenyekiti wake, Clement Sanga, umewapiga ‘stop’ wachezaji wa timu hiyo kuzungumzia masuala ya kadi tatu za njano yanayomhusu beki wa Kagera Sugar, Mohammed Fakhi.

Fakhi alikatiwa rufaa na Simba kwa kile kinachodaiwa kuwa aliichezea timu yake ya Kagera akiwa na kadi tatu za njano mchezo ambao Kagera walipata ushindi wa mabao 2-1.

Hata hivyo, baadaye Kamati ya Saa 72 ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), iliipa Simba ushindi kwenye mchezo huo, jambo ambalo limekuwa likilalamikiwa na mashabiki wa soka nchini.

Uongozi wa Yanga wenyewe umesema kuwa hautaki kuwaona wachezaji wao wakijadili kuhusu kadi hizo bali waendelee kupambana uwanjani kwani wakishinda michezo yao yote bado wanaweza kuwa mabingwa.

Akizungumza na Championi Jumatano, Sanga alisema kuwa haoni sababu ya Msuva au mchezaji yeyote wa Yanga kwa kipindi hiki kujadili mambo ya Simba na Kagera Sugar wakati mambo hayo si ya Yanga bali ni ya kamati za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na walalamikaji husika.

“Kweli kwa sisi tusingependa sana kwa kipindi hiki kumuona mchezaji yeyote wa Yanga akitumia muda wake mwingi kuwazia mambo ya kadi tatu za Fakhi au kuanza kulijadili suala hilo.

“Maana tungependa kuelekeza mawazo na akili zetu katika michezo iliyosalia, kwani matokeo yanaweza kupatikana uwanjani tu na siyo sehemu nyingine,” alisema Sanga.

Download App Yetu MPYA  >> BOFYA HAPA << Tukutumie Habari na Burudani Zote FASTA Kila Siku !

No comments

TOA MAONI YAKO HAPO CHINI.