Yanga ilivyojiua yenyewe Algeria - BongoSwaggz.Com

Advert

Breaking News

Yanga ilivyojiua yenyewe Algeria

USHINDI finyu wa bao 1-0 ambao Yanga iliupata katika mechi ya kwanza iliyofanyika Aprili 8, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa dhidi ya MC Alger ndiyo ilikuwa tiketi ya 'kwaheri' kwa wawakilishi hao pekee wa Tanzania waliokuwa wamebakia katika mashindano ya kimataifa, imeelezwa.

Yanga iliiaga michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kupata kichapo cha mabao 4-0 na kufanya matokeo ya jumla kuwa 4-1 dhidi ya wenyeji wao MC Alger ya Algeria.

Akizungumza na gazeti hili jana, mchambuzi wa soka na kocha wa zamani wa timu hiyo, Kenny Mwaisabula, alisema kuwa MC Alger walificha mbinu zao walipokuwa hapa nchini na hiyo iliwafanya Yanga washindwe kuwafahamu vyema.

Mwaisabula alisema kuwa kiwango cha soka walichokionyesha wachezaji wa MC Alger juzi wakiwa nyumbani kwao, kilikuwa ni cha juu na kiliwafanya Yanga washindwe kuelewana katika dakika zote 90 za mchezo huo.

"Waarabu wanajua kujipanga, wanajua kutumia vyema uwanja wa nyumbani, wao ugenini huja na mkakati wa kutafuta sare au ushindi mdogo, lakini wanapofika kwao hali huwa ni tofauti, hawana kawaida ya kucheza soka lao la asili ugenini," alisema Mwaisabula.

Aliongeza kuwa matatizo ya nje ya uwanja kamwe hayahusiani na mchezo huo kwa sababu wachezaji wanapaswa kufahamu soka ndiyo ajira yao ambayo wanaitegemea.

Naye Katibu Mkuu wa zamani wa Yanga, Jonas Tiboroha, alisema kuwa kuondolewa kwa timu hiyo kwenye michuano ya kimataifa ni matokeo ya kiwango cha chini cha ligi ya Tanzania.
"Hii ndiyo taswira ya kiwango chetu," alisema kwa kifupi Tiboroha ambaye alijiuzulu Yanga baada ya kutofautiana na viongozi wa juu wa klabu hiyo mwaka jana.

Yanga ilitarajiwa kurejea jana nchini na kuanza maandalizi ya mechi yake ya hatua ya robo fainali ya mashindano ya Kombe la FA dhidi ya Tanzania Prisons itakayofanyika Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa.

Download App Yetu MPYA  >> BOFYA HAPA << Tukutumie Habari na Burudani Zote FASTA Kila Siku !

No comments

TOA MAONI YAKO HAPO CHINI.