Simba: Hatuwezi kufungwa na Azam - BongoSwaggz.Com

Advert

Breaking News

Simba: Hatuwezi kufungwa na Azam

HATUFUNGWI! Hiyo ni kauli ya Meneja wa Simba, Mussa Hassan 'Mgosi' baada ya kufunguka kuwa kikosi chake kinaendelea vizuri na mazoezi kwenye kambi yao iliyopo Morogoro na kutamba hawako tayari kuona wanafungwa mara mbili mfululizo na Azam FC.

Mapema mwaka huu Azam FC iliwafunga Simba katika mechi ya fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi iliyofanyika Zanzibar na pia ikawalaza kwenye mechi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Simba na Azam FC zitakutana katika mechi ya hatua ya nusu fainali ya Kombe la FA itakayofanyika keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mgosi, alisema mbali na mazoezi ya uwanjani, pia wanaziangalia mechi mbalimbali za Azam ili waweze kufahamu uimara na mapungufu ya wachezaji wake na hatimaye kupanga mbinu za kuwadhibiti.

Mgosi alisema watahakikisha wanaongeza umakini kwenye mchezo huo ambao mshindi atafanikiwa kutinga hatua ya fainali ya mashindano hayo yanayotoa mwakilishi wa Tanzania Bara kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.

"Itakuwa ngumu kufungwa mara mbili, wataingia wakijiamini na sisi tutaingia tumejipanga kuwadhibiti, mechi itakuwa na mvuto, ushindani, lakini hatutakubali kuipoteza," alisema mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba, JKT Ruvu na Mtibwa Sugar zote za Tanzania.

Meneja huyo alisema pia beki Method Mwanjali leo ataanza mazoezi ya pamoja na wachezaji wenzake baada ya kumaliza programu maalumu iliyokuwa chini ya maelekezo ya daktari wa timu hiyo.

"Nafasi yake ya kucheza au kutokucheza bado haiko wazi, alikuwa anafanya mazoezi peke yake, lakini kuanzia kesho (leo) atajumuika na wenzake," Mgosi alisema.

Baada ya mechi hiyo, Simba itarejea Dar es Salaam kuendelea na maandalizi ya kumaliza michezo yake mitatu iliyobakia ya Ligi Kuu Bara dhidi ya African Lyon, Stand United na Mwadui FC.

Download App Yetu MPYA  >> BOFYA HAPA << Tukutumie Habari na Burudani Zote FASTA Kila Siku !

No comments

TOA MAONI YAKO HAPO CHINI.