Rais Magufuli Aagiza TCU kuacha kuchagulia vyuo wanafunzi - BongoSwaggz.Com

Advert

Breaking News

Rais Magufuli Aagiza TCU kuacha kuchagulia vyuo wanafunzi

Rais John Magufuli ameiagiza Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kutowachagulia vyuo wanafunzi wa elimu ya juu na kuwaacha wanafunzi hao kuchagua vyuo wanavyovitaka wenyewe.

Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Rais Magufuli alipokuwa akizindua mabweni ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambapo alikitaka chuo hicho pia kutoza Sh 500 kwa siku tofauti na Sh 800 ambazo zinatoswa kwa hosteli nyingine.

“Ninaamini kama wanafunzi wangepewa nafasi ya kuchagua vyuo wanavyovipenda wenyewe, vyuo vya Serikali kama vile Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Chuo Kikuu cha Mzumbe vingekuwa na wanafunzi wengi sana,” alisema Magufuli.

Aliendelea kwa kusema kuwa TCU imekuwa ikiwachagulia wanafunzi vyuo visivyo na sifa na makazi ya wanafunzi hivyo kusababisha wanafunzi hao kusoma katika mazingira magumu na wanapomaliza masomo yao hukosa ajira kutokana na vyuo hivyo kutokuwa na sifa. Rais Magufuli alitaka Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) lenyewe kubaki na udhibiti.

Aidha alisema ni vyema Tume ikabaki na majukumu yake kama kuhimiza ubadilishaji wa maarifa/elimu kwa njia ya kuunganisha kimtandao Vyuo Vikuu na Vyuo vya Vyuo Vikuu, usajili na utambuzi rasmi wa Vyuo Vikuu na Vyuo vya Vyuo Vikuu, uthibitishaji wa programu za kitaaluma, uthibitishaji na uratibu wa udahili wa wanafunzi.

Majukumu mengine ni ufuatiliaji na udhibiti wa elimu bora Vyuo Vikuu na Vyuo vya Vyuo Vikuu, ukusanyaji na usambazaji wa taarifa/ data kuhusu elimu ya juu. “Niombe tu kwa Wizara ya Elimu na TCU tubadilishe kidogo utaratibu wa kuchagulia wanafunzi, wanafunzi wawe wanachagua vyuo badala ya TCU kuwachagulia vyuo vya kwenda,” alisema. Akifafanua zaidi alisema kama wanafunzi wakijichaguliwa vyuo, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kingejaa wanafunzi 23,000 wanaotakiwa kuwepo katika chuo hicho.

“Lakini sijajua ni kwa nini mtu amefaulu anataka kuja hapa afaidi mabweni ya Magufuli analazimishwa kwenda kwenye kachuo ambako hakana jina akasome pale, wakati hakuna hata mabweni, saa nyingine hata walimu hawana, tunawatesa watoto hawa,” alisema. Alisema anafahamu ingawa hana ushahidi kuwa wakuu wa vyuo hivyo wanatoa fedha kwa viongozi wa TCU ili wapangiwe idadi ya wanafunzi wanaowahitaji kwenye vyuo vyao.

Rais Magufuli alisema kuwa TCU ibaki kuwa mdhibiti wa elimu lakini wanafunzi wabaki kuwa na haki ya kuchagua vyuo kwani baadhi ya vyuo vinaendesha shughuli zake kwa mikopo ya wanafunzi hao. “Tuwaache watoto wachague vyuo wanavyovitaka, vile ambavyo havitachaguliwa, vife kwanini mnalazimisha vyuo ambavyo havina ubora vipate wanafunzi msipolazimisha vyuo ambavyo vina ubora vitapata watu….. najua maneno haya hayawafurahishi baadhi ya watu na mimi siko hapa kumfurahisha mtu?” alisema Rais Magufuli.

Awali Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandara, alisema mradi huo una majengo 20, kila jengo lina gorofa nne na ujenzi wake umekamilika ndani ya miezi minane. Majengo hayo yatachukua wanafunzi 3,840.

Akizungumzia mradi huo wa majengo ya mabweni, Rais Magufuli alisema anafuraha kukamilika majengo hayo kwa sababu ahadi yake imetimia “Yale niliyoyaahidi yametimia, chuo kikuu kimekuwa na matatizo ya makazi kwa ajili ya vijana wetu, matatizo haya ni ya siku nyingi na tumekuwa hatuyaangalii sana kwa sababu yanawahusu wanafunzi hayatuhusu sisi,” alisema Rais Magufuli.

Alisema vijana wengi wanapochaguliwa kuingia chuo kikuu huwa hawajui kuwa kuna tatizo hilo wengine kuishia kupanga vyumba mitaani na wengine kubebana katika mabweni huku kitanda kimoja kikichukua zaidi ya wanafunzi watatu. Rais Magufuli alisema kuwa kutokana na tatizo hilo la makazi kwa wanafunzi wapo vijana wengine wameamua kuoa na kuolewa ili tu waweze kupata sehemu za kuishi.

Alisema chuo hicho ndio chuo kikuu mama katika historia ya nchi na kwamba viongozi wengi wamesoma katika chuo hicho. Rais Magufuli alisema kwa kutambua tatizo hilo aliahidi kutafuta Sh bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni ya chuo hicho ingawa hakuwa na uhakika wa kufanikiwa lengo lake hilo. “Niliwaita wataalamu nilipowapa ramani wakasema majengo hayo yatagharimu Sh bilioni 150 hadi bilioni 200, hapo unaweza kujiuliza wewe umetenga Sh bilioni 10 unaambiwa inayoweza kutosha ni Sh bilioni hizo, ilikuwa ni lugha ya kukatisha tamaa,” alisema Rais Magufuli.

Alisema hakukata tamaa akaamua kumuita Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Elius Mwakalinga alipopiga hesabu akamwambia Sh bilioni 10 zingetosha katika ujenzi huo. Katika ujenzi huo Rais Magufuli alisema aliihusisha pia Wizara ya Ulinzi kusimamia na pia JKT katika ujenzi wa uzio wakati watu wengine wakishiriki ujenzi huo na pia alikiomba chuo kutoa eneo.

Rais Magufuli alipongeza uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kufanya maamuzi ya kutoa eneo hilo ambapo awali ilishindikana kutumia maeneo hayo na kwenda kujengwa mabweni eneo la Mabibo ambapo ni mbali na chuo hicho. Alisema mabweni ya Mabibo yalijengwa mwaka 2000 kwa gharama ya Sh bilioni 27, yanachukua wanafunzi 4,000, lakini mabweni hayo yaliyojengwa sasa yanachukua wanafunzi 3,840 na gharama yake ni Sh bilioni10.

Rais Magufuli alisema kwa mfano uliooneshwa na TBA iwe fundisho kwa viongozi wa serikali ambao wamezoea zauni zenye gharama kubwa kwa manufaa yao na sio manufaa ya Serikali. “Hii iwe fundisho kwa watumishi na viongozi wa serikali waliozowea kuchukua ten pasenti na wakati mwingine 70 pasenti kwa majengo ambayo yangeweza kujengwa kwa gharama kidogo, pili iwe fundisho kwetu kuamini wakandarasi wa ndani wanaweza,” alisema Rais Magufuli.

Alisema wapo watu ambao hawaamini kuwa watanzania wanaweza kujenga vizuri kama ambavyo imefanyika katika mradi huo, “napenda nitoe wito kwa watanzania, vizuri vinafanywa na watanzania.” Rais Magufuli alisema wapo watu ambao walibeza kuwa kwa gharama ya Sh bilioni 10 isingewezekana kujengwa nyumba hizo ambapo wakiona mradi umekamilika wanashangaa.

“Kwahiyo nawashukuru sana TBA, Mwakalinga umefanya kazi nzuri sana, Bodi ya TBA mmefanya kazi nzuri, mabweni haya mazuri yamekamilika kwa kipindi kifupi inadhihirisha Tanzania tunaweza, tukiamua tunaweza na watu wakaona ni miujiza,” alisema. Rais Magufuli alisema bila ulinzi uliofanywa na jeshi gharama zingekuwa kubwa lakini walilinda vizuri na pia alipongeza Suma JKT kwa kujenga ukuta wa uzio na kumaliza kwa wakati mfupi.

Aidha Rais Magufuli aliupongeza uongozi wa chuo hicho kwa kutimiza ahadi yake ya kuweka kwenye mabweni hayo vitanda na makabati, ambapo amewaasa wanafunzi watakaotumia mabweni hayo wayatumie na kuyatunza. Katika suala la bei, Rais Magufuli aliutaka uongozi wa chuo hicho tofauti na inavyolipishwa kwa mabweni mengine kiwango cha Sh 800 mabweni hayo wanafunzi walipe Sh 500 kwa siku.

“Nafahamu suala la bei, wanafunzi hua wanalipa Sh 800, sasa Sh 800 sijui aliyejenga mabweni hayo, hapa walipe Sh 500 si nimejenga mimi pesa inayobaki wanunue kalamu wakae wasome, na ninaamini watayatunza mabweni haya,” alisema. Rais Magufuli alisema serikali yake imeamua kuwekeza katika elimu na hasa kwa watoto wa masikini ili waweze kupata elimu na kuongeza pia mikopo imeboreshwa. Aliagiza pia uongozi wa chuo hicho kununua mabasi kwa ajili ya kubeba wanafunzi kutoka mabweni yaliyo mbali na chuo hicho.

Rais Magufuli alimpongeza Katibu Mkuu wa Maji na Umwagiliaji Kitila Mkumbo ambaye amemteua hivi karibuni kwa kwenda CCM na kuuliza ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) inavyosema katika suala la maji na sasa ameanza kufanya kazi.

Hata hivyo Rais Magufuli alikitaka chuo hicho kuwaachia wanafunzi ambao wanasoma masomo ya afya katika chuo hicho kwenda kwenye Hospitali ya Mloganzila ambayo inatarajiwa kufunguliwa hivi karibuni na wengine kupelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambazo ndizo zinazojihusisha na masomo ya afya kwa vitendo.

Awali Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Profesa Joyce Ndalichako alimfahamisha Rais Magufuli kuwa hospitali hiyo iko tayari na hivi karibuni watamuomba kwenda kuzindua. Aidha Profesa Ndalichako alimpongeza Rais Magufuli kutimiza ahadi zake kwa vitendo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa mabweni hayo pamoja na kuboresha sekta nzima ya elimu ambapo alitoa onyo kwa watumishi wengine ambao wanajenga chumba kimoja cha darasa kwa miaka miwili na kwa gharama kubwa.

Download App Yetu MPYA  >> BOFYA HAPA << Tukutumie Habari na Burudani Zote FASTA Kila Siku !

No comments

TOA MAONI YAKO HAPO CHINI.