Pointi tatu za Simba Kagera mezani leo - BongoSwaggz.Com

Advert

Breaking News

Pointi tatu za Simba Kagera mezani leo

KIKOSI CHA SIMBA.

HATIMA ya rufaa iliyokatwa na Klabu ya Simba dhidi ya Kagera Sugar ambayo ilimchezesha beki wake Mohammed Fakhi akiwa na kadi tatu za njano, inatarajiwa kujulikana leo baada ya kikao cha Kamati ya Saa 72 ya Usimamizi wa Ligi Kuu itakapokutana.

Katika mechi hiyo ya Ligi Kuu Tanzania Bara namba 194, iliyofanyika Aprili 2, mwaka huu kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, Simba ilikubali kichapo cha mabao 2-1.

Taarifa kutoka kwa kiongozi mmoja wa bodi ya ligi (jina tunalihifadhi) ilieleza jana kuwa, kikao hicho kitafanyika leo kama ilivyopangwa na uamuzi juu ya rufaa hiyo utatolewa baada ya kikao hicho kumalizika.

'Kikao kipo kama ilivyoelezwa, tayari maandalizi na nyaraka muhimu ambazo zilihitajika zimeshawasili, wajumbe wote wanaohusika wameshataarifiwa juu ya kuhudhuria kikao hicho," alisema kiongozi huyo wa bodi ya ligi.

Kiongozi huyo alisema kuwa mbali na rufaa hiyo ya Simba, pia kikao hicho kitajadili taarifa za mechi nyingine mbili za ligi hiyo zilizofanyika juzi kwenye viwanja viwili tofauti hapa nchini.

"Kikao kitajadili pia taarifa za mechi za juzi (Jumatatu) kati ya Mbao FC dhidi ya Simba na mchezo wa Mtibwa Sugar dhidi ya Azam FC, si unajua lazima nazo zijadiliwe kabisa kwa sababu tayari taarifa zimeshatumwa," aliongeza kiongozi huyo.

Mechi ambazo Fakhi anadaiwa alionyeshwa kadi za njano ni ile iliyofanyika Desemba 17, 2016 katika mchezo namba 122 kati ya Mbeya City dhidi ya Kagera Sugar uliopigwa Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya na nyingine ilikuwa ni Januari 18, mwaka huu kwenye Uwanja wa Kaitaba, walipokipiga dhidi ya African Lyon ya Dar es Salaam.

Machi 4, mwaka huu Fakhi alionyeshwa kadi nyingine ya tatu katika mchezo namba 190 kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba wakati Kagera ilipoikaribisha Majimaji ya Songea.

Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime, alikaririwa na vyombo vya habari kuwa mchezaji huyo alikuwa na kadi mbili za njano na si tatu kama Simba wanavyodai.

Download App Yetu MPYA  >> BOFYA HAPA << Tukutumie Habari na Burudani Zote FASTA Kila Siku !

No comments

TOA MAONI YAKO HAPO CHINI.