Mbao yashikilia rufaa ya Simba - BongoSwaggz.Com

Advert

Breaking News

Mbao yashikilia rufaa ya Simba

Rufaa ya Simba dhidi ya Kagera Sugar inaweza kuwa na kuongezeka au kupoteza thamani yake kutokana na matokeo yatakayopatikana leo dhidi ya Mbao FC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Simba ilikata rufaa hiyo muda mfupi baada ya kupoteza mechi dhidi ya Kagera Sugar kwa mabao 2-1, ikiituhumu kumtumia beki Mohammed Fakhi, huku akiwa na kadi tatu za njano, kinyume na kanuni za Ligi Kuu Bara.

Huku ikishika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 55 nyuma ya Yanga yenye 56, Simba inawania pointi tatu zitakazoifanya iwe mbele ya Yanga kwa pointi mbili na iwapo ikishinda rufaa yake, itafikisha pointi 61, tano mbele ya Yanga, ambayo ina faida ya mchezo mmoja mkononi.

Lakini, iwapo itapoteza dhidi ya Mbao au kutoka sare, ni wazi kuwa Simba itajiweka pagumu kwenye mbio za ubingwa hata kama itashinda rufaa yake, kwani bado itakuwa nyuma ya Yanga, ambayo inaweza kutumia vizuri faida ya mechi iliyonayo mkononi kujitengenezea mazingira ya kutetea taji la Ligi Kuu kwa mara ya tatu.

Tangu ilipoibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Toto Africans, Januari 31, 2010, Simba inatimiza miaka saba na miezi miwili (siku 2,726) pasipo kupata ushindi kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, ingawa imebahatika kupata matokeo ya sare mara kadhaa.

Benchi la ufundi la Simba limewapa angalizo nyota wake kusahau matokeo yaliyopatikana kwenye mechi dhidi ya Kagera Sugar na kutotilia maanani rufaa ambayo wamekata na badala yake watafute pointi tatu.

“Kwanza tunapaswa kuhakikisha tunapata pointi dhidi ya Mbao, halafu hayo mambo mengine yatajulikana baadaye, lakini tukisema tuyafuatilie kwa sasa tutazidi kujipoteza,” alisema kocha msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja.

Kocha wa Mbao FC inayoshika nafasi ya 12 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 27, Etienne Ndayiragije alisema ushindi dhidi ya Simba utakuwa na faida kubwa kwao na utawaweka mahali pazuri.

“Hatuko kwenye nafasi nzuri na mbinu pekee ya kutoka hapa tulipo kwenye msimamo ni kupata ushindi dhidi ya Simba na si vinginevyo,” alisema Ndayaragire.    

Download App Yetu MPYA  >> BOFYA HAPA << Tukutumie Habari na Burudani Zote FASTA Kila Siku !

No comments

TOA MAONI YAKO HAPO CHINI.