Kila la heri Yanga, tutoeni Watanzania kimasomaso - BongoSwaggz.Com

Advert

Breaking News

Kila la heri Yanga, tutoeni Watanzania kimasomaso

WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, Yanga, leo wanajitupa uwanjani jijini Algiers, Algeria kupambana na MC Alger katika mchezo wa marudiano.


Mabingwa hao wa Tanzania Bara wanaingia uwanjani kutupa karata ya kutafuta nafasi ya kushiriki katika hatua ya makundi kwenye michuano hiyo inayoandaliwa na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF).

Wakati wawakilishi hao wa Tanzania kwenye michuano hiyo wakiwa katika kibarua hicho kigumu, tayari wana hazina ya ushindi wa bao moja walilolipata katika mchezo wa kwanza uliofanyika katika uwanja wa Taifa, Dar es salaam, baada ya kuwashinda wapinzani hao bao 1-0.

Kutokana na hazina hiyo, Yanga inahitaji sare ya aina yoyote ile ili isonge mbele na kuingia katika mtifuano wa makundi ambao utajumuisha timu nane, nne kutoka kila kundi. Iwapo itafanikiwa kuvuka kihunzi cha leo, itaingia katika hatua hiyo kwa mara ya pili mfululizo baada ya msimu uliopita kufika hatua hiyo licha ya kwamba haikufanya vizuri.

Kama alivyosema Kocha msaidizi Juma Mwambusi kwamba wanakwenda Algeria kushindana kisha kusonga mbele, Yanga wanapaswa kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha wanafanya vizuri na hatimaye kuwatoa kimasomaso Watanzania katika michuano ya kimataifa.

Tunasema hivyo kwa sababu kwa miaka mingi timu za Tanzania zimekuwa hazifanyi vyema kwenye michuano hiyo kwani nyingi huishia katika hatua za awali na kama zinavuka, kama ilivyo kuwa kwa Yanga mwaka jana, hufanya vibaya.

Katika ulimwengu wa soka, siku zote hakuna lisilowezekana hivyo Yanga wanapaswa kuondokana na hofu na dhana iliyojengeka miongoni mwa Watanzania kuwa timu za kaskazini mwa Afrika zimekuwa zikizisumbua timu za Tanzania na hata kuzifungisha virago kwenye michuano mbalimbali.

Historia inaonyesha kuwa timu za Tunisia, Algeria, Morocco na Misri zimekuwa zikizisumbua timu za Tanzania na pia kumekuwa na imani kwamba timu zetu hufanyiwa fitina kwa kuanza mechi nyumbani na kumalizia ugenini ili kuweka mazingira ya kuondoshwa kwenye michuano hiyo.

Kwa jumla imani hiyo kwa muktadha wa soka la sasa haina mashiko sana kwa sababu hakuna sababu ya mazingira ya nyumbani wala ugenini ili kushinda bali dawa kubwa ni maandalizi katika mchezo husika.

Tunasema hivyo kwa sababu hiyo si kanuni ya ushindi bali kinachotakiwa ni kujiandaa na hatimaye kushinda.

Inachotakiwa kufanya Yanga ni kuhakikisha inacheza kwa ari na umoja ili kushinda mechi ya leo. Kama wapinzani wao walivyoonekana katika mechi ya awali ya Jumamosi iliyopita, Yanga ina uwezo wa kuleta matokeo chanya leo na hatimaye kusonga mbele.

Sambamba na hilo, viongozi na benchi la ufundi la Yanga wanatakiwa kuwaandaa kisaikolojia wachezaji wao kwa mchezo huo ili kushinda badala ya kuwaongezea hofu kwamba Waarabu ni wagumu kufungika wakiwa katika viwanja vyao vya nyumbani.

Shime Yanga watoeni Watanzania kimasomaso kwa kuiondoa MC Alger na kusonga mbele. Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Yanga.

Download App Yetu MPYA  >> BOFYA HAPA << Tukutumie Habari na Burudani Zote FASTA Kila Siku !

No comments

TOA MAONI YAKO HAPO CHINI.