Hizi Ndio Sababu za Waziri Mwakyembe Kushindwa Kuwapatanisha Diamond na Ali Kiba..!!! - BongoSwaggz.Com

Advert

Breaking News

Hizi Ndio Sababu za Waziri Mwakyembe Kushindwa Kuwapatanisha Diamond na Ali Kiba..!!!

BAADA ya Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk. Harrison George Mwakyembe kutamka hadharani kuwa na mipango ya kuwapatanisha wakali wa Muziki wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’, sababu sita zitakazomfanya waziri huyo kugonga mwamba, zimeelezwa IMEKUJAJE?

Hivi karibuni Waziri Mwakyembe akiwa mkoani Dodoma alizungumza na waandishi wa habari akitoa wito kwa Watanzania kuichangia Timu ya Taifa ya Vijana Chini ya Miaka 17 (Serengeti Boys) huku akitaja listi ya wadau mbalimbali wanaoongoza hamasa hiyo.

Miongoni mwa watu aliowapongeza walikuwa ni Diamond na Kiba na kusema kuwa, amefurahishwa kuwepo kwao katika hamasa hiyo na kuwataka kukutana nao Dodoma mara moja kwani anasikia kuwa hawakai pamoja na kuongeza kwamba, yeye ni kama baba yao hivyo lazima watakaa pamoja (kuelewana).

Kutokana na tamko hilo, vyanzo vya karibu na wakali hao, vimetonya kuwa, jambo hilo haliwezekani huku sababu sita (6) zitakazomfanya Waziri Mwakyembe kugonga mwamba;

SABABU YA KWANZA

Mmoja wa vyanzo vya karibu na wawili hao, alitoa sababu ya kwanza kuwa ni kujitengenezea fedha. Kwamba kuendelea kuwa na bifu kutawafanya kuendelea kuwa na ushindani hivyo ni jambo lililokaa kibiashara hivyo hawapo tayari kupoteza fursa hiyo.

“Hivi karibuni Diamond alifungua tovuti ya Wasafi.com ambayo imekusanya karibu nusu ya wasanii wa muziki wakubwa nchini, wanauza kazi zao huko kwa makubaliano na fedha kidogo zinaingia kwake nyingine kwa wasanii hao. Diamond amekuwa akitamka kuwa anapenda na Kiba ajiunge nao.
“Kiba naye amekuwa mgumu wa kukubali kwa maana ameshaona kuwa kupeleka nyimbo zake Wasafi. com, kwanza kutaliua bifu lao linalomsaidia vitu vingi vya faida na pili atakuwa chini ya Diamond ambapo atakuwa kama anamtengenezea fedha mtu ambaye anashindana naye kwenye biashara ya muziki.

Kutokana na tamko hilo, vyanzo vya karibu na wakali hao, vimetonya kuwa, jambo hilo haliwezekani huku sababu sita (6) zitakazomfanya Waziri Mwakyembe kugonga mwamba;


SABABU YA PILI

Chanzo hicho kilizidi kutiririka kuwa, sababu ya pili itakayomfanya Waziri Mwakyembe kugonga mwamba ni mameneja wa wasanii hao kutoshirikiana kwa ukaribu.

“Tangu nimemfahamu Diamond akiwa chini ya Babu Tale na Sallam SK sijawahi hata siku moja kuwaona kwenye meza moja wakitafuta suluhu na meneja wa Kiba, Seven.

Hawajawahi hata kushirikiana wala kuandaa shoo ya pamoja na inapotokea shoo wakapangiwa pamoja lazima mmojawapo atakataa au kuweka masharti magumu au kufanyiana fitina.

“Ipo mifano mingi inayoonesha wazi hawaivi chungu kimoja. Kama utakumbuka katika Tamasha la Rock lililofanyika Viwanja vya Golf, Mombasa mwaka jana likimshirikisha staa kutoka Marekani, Christopher Maurice ‘Chris Brown’, Kiba naye alikuwa mgeni mwalikwa ambaye alipafomu lakini liligeuka kuwa na sintofahamu baada ya Kiba kupanda na kupafomu nyimbo mbili tu, ikiwemo Mac Muga kisha kuzimiwa kipaza sauti na baada ya kushuka malalamiko aliyaelekeza kwa Meneja wa Diamond, Sallam kuwa amefanya yote hayo,” kilisema chanzo hicho.

SABABU YA TATU

Sababu ya tatu inaelezwa kuwa ni kukwepana wasanii hao kwa muda mrefu pindi wanapoandaliwa matamasha au linapotokea jambo la kuwakutanisha.

“Kwa muda mrefu Kiba na Diamond wamekuwa wakikwepana na ukweli huu upo wazi kwa mashabiki wao. Walishawahi kukwepana mwaka 2015 katika Viwanja vya Leaders jijini Dar katika moja ya shoo iliyoandaliwa na Kampuni ya Mawasiliano ya Tigo ikitambulika kama Tigo Kiboko Yao ambapo Kiba hakutumia mlango maalum wa VIP (aliruka fensi) kuingia ndani kwenye eneo la wasanii wenzake akiwemo Diamond.

“Mwaka jana katika sherehe ya kutimiza miaka 10 ya Chama cha Orange for Democratic Movements (ODM) cha Raila Odinga, Kiba na Diamond walialikwa bila kujuana katika Viwanja vya Mama Ngina, Mombasa kutokana na kutokuelewana kwao. Kilichotokea usiku huo, Diamond alitangazwa kama msanii rasmi atakayetumbuiza akafanya hivyo na baada ya hapo Kiba naye aliingia kama msanii wa sapraizi, jambo lililofanya shangwe kuzidiana na kuonekana kama mmoja amefunikwa,” kilisema chanzo chetu.

SABABU YA NNE

Chanzo kingine cha karibu na wasanii hao kiliongeza kuwa sababu nyingine ambayo ni ngumu kwa waziri huyo kuwapatanisha ni kila mmoja kutaka kuendelea kuwa kileleni. “Diamond ni msanii mkubwa sawa na Kiba, kumekuwa na ushindani sana kila mmoja kuendelea kukaa kileleni kwa kutoa nyimbo kali, ndiyo maana umesikia Kiba amesainiwa na Sony Music Africa na wakati
huohuo Diamond naye ameingia saini na Lebo ya Universal Music Group kusambaza kazi zake na za lebo yake,” kilisema chanzo hicho ambacho ni mchambuzi wa masuala ya burudani na mastaa Bongo.

SABABU YA TANO Ilifahamika kuwa, sababu nyingine kubwa inayoleta ugumu wa wawili hao kupatana ni kuundwa kwa timu (team) ambazo zimekuwa zikigandamizana kimuziki. Kiba ana team yake (Team Kiba) na Diamond (Team Diamond). “Team zote hizi zimekuwa zikilikoleza bifu la Diamond na Kiba na kufanya kuwa ngumu kupatana.

Kama kweli waziri anataka kuwapatanisha, angeanza kudili na makundi haya. Mfano inapotokea Diamond akapata tuzo au akafanya vizuri sehemu f’lan ni wazi timu hizi zitaanza kupondana. Inasemekana kuwa, imefikia hatua hata wawili hao wanapochaguliwa katika tuzo za kimataifa wakiwa kipengele kimoja au mmojawapo akichaguliwa kushiriki basi hizi timu hushirikiana kuuangusha upande wa pili,” kiliendelea chanzo hicho.

SABABU YA SITA Sababu ya sita na ya mwisho iliyotajwa kuleta ugumu wa kuwapatanisha wawili hao ni kutokuwa tayari. Kila mmoja kwa upande wake akihojiwa husema kuwa hana tatizo na mwenzake japokuwa kuna kinyongo wamejiwekea.

“Diamond na Kiba wenyewe hawajawa na utayari wa kupatana. Ukikaa na Kiba atakuambia hana bifu naye na Diamond vivyohivyo. Ujue hawa wana kinyongo tangu wafutiane nyimbo. Diamond alimfuta Kiba katika Wimbo wa Lala Salama na Kiba naye akalipiza kumfuta katika Wimbo wa Single Boy,” kilimaliza chanzo.

MTAZAMO WA DULLY Kuhusu kupatana kwa Diamond na Kiba, staa ambaye ni mkongwe katika Bongo Fleva, Dully Sykes alikaririwa akisema kuwa, kwa sasa wasanii hao kupatana ni jambo gumu mpaka atakapotokea msanii atakayewazidi na kuwa kileleni kwa kila kitu zaidi yao.

Download App Yetu MPYA  >> BOFYA HAPA << Tukutumie Habari na Burudani Zote FASTA Kila Siku !

No comments

TOA MAONI YAKO HAPO CHINI.