Hakuna njaa, kuna uhaba wa fedha -Tizeba - BongoSwaggz.Com

Advert

Breaking News

Hakuna njaa, kuna uhaba wa fedha -Tizeba

WAZIRI wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba amebainisha kuwa kwa sasa Tanzania hakuna tatizo la njaa kutokana na masoko mengi kuwa na chakula isipokuwa tatizo lililopo ni uhaba wa fedha.

Waziri Tizeba aliyasema hayo alipokutana na baadhi ya wananchi kwenye maeneo ya soko kuu mjini Shinyanga alipopita akienda mkoani Dodoma kuendelea kushiriki katika vikao vya Bunge la bajeti vinavyoendelea mkoani humo.

Tizeba alitolea ufafanuzi suala la madai ya kuwepo kwa njaa katika baadhi ya maeneo hapa nchini na kufafanua kuwa kinachodaiwa ni njaa ni uhaba wa fedha kwa baadhi ya watu kwa vile tafiti zilizofanywa na serikali katika maeneo mengi zimeonesha uwepo wa chakula katika masoko mengi.

“Wananchi wenzangu si kweli hapa nchini tuna janga la njaa, nasema kwa ushahidi ninyi wenyewe tembeleeni maeneo mbalimbali katika masoko yetu mtajionea hali halisi, vyakula ni vingi tatizo ni uhaba wa fedha kwa baadhi ya watu, sasa hii huwezi kusema ni njaa,” alisema.

Alisema wapo baadhi ya wanasiasa wanaishinikiza serikali itoe chakula cha akiba ili kigawiwe bure au kiuzwe kwa bei nafuu kwa wananchi, jambo ambalo ni kukurupuka kwani kikiuzwa kwa bei rahisi kitakapomalizika wafanyabiashara watapata mwanya wa kuuza vyakula walivyonavyo kwa bei kubwa.

Kuhusu suala la uwepo wa wadudu waharibifu wa mazao katika maeneo mengi nchini, waziri huyo alisema tatizo hilo linachangiwa na ugumu wa kukabiliana na wadudu hao kutokana na mashamba mengi kulimwa kwenye maeneo ya makazi ya watu.

“Tunawashauri wakulima wetu kwa hili hakuna sababu ya kusubiri serikali, waungane watatu ama watano wanunue vifaa pamoja na dawa za kuulia wadudu hawa, bei si kubwa wanaweza kunyunyuzia kwa kupeana zamu, sisi serikali tutafanya kazi hii kwenye mashamba makubwa,” alisema.

Hata hivyo alikiri kuwepo kwa ongezeko la bei ya sukari katika maeneo mengi nchini kwani kwa mujibu wa taarifa za wiki iliyopita baadhi ya maeneo kilo moja ya sukari ilikuwa ikiuzwa kwa Sh 3,000, hali iliyochangiwa na viwanda kusimamisha uzalishaji kipindi hiki cha masika.

Download App Yetu MPYA  >> BOFYA HAPA << Tukutumie Habari na Burudani Zote FASTA Kila Siku !

No comments

TOA MAONI YAKO HAPO CHINI.