Gwajima kujitetea kortini leo - BongoSwaggz.Com

Advert

Breaking News

Gwajima kujitetea kortini leo

KESI ya kushindwa kuhifadhi silaha inayomkabili Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima na wenzake itaendelea kunguruma leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ambapo washitakiwa hao watajitetea.

Wakili wa Serikali, Joseph Maugo alidai jana mbele ya Hakimu Mkazi, Godfrey Mwambapa kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kusikiliza na kwamba upande wa mashitaka upo tayari kuendelea.

Hata hivyo, Hakimu Mwambapa alisema hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Thomas Simba hayupo hivyo itaendelea kusikilizwa leo.

Mbali na Gwajima, washitakiwa wengine ni Askofu Msaidizi wa kabisa hilo, Yekonia Bihagaze, mfanyabiashara George Mzava na mkazi wa Kimara Baruti, Geoffrey Milulu.

Washitakiwa hao wanadaiwa walikutwa na begi likiwa na vitu mbalimbali ikiwamo risasi 17 na bastola. Awali, katika utetezi wake, Gwajima alidai kuwa Machi 27, 2015 alikuwa safarini kuelekea Arusha kwenye kikao cha maaskofu, na aliondoka Dar es Salaam, Machi 26, 2015.

Alidai kuwa wakati alipokuwa njiani kuelekea Arusha aliona taarifa kwenye mtandao wa kijamii kuwa Askofu Gwajima anatafutwa na Jeshi la Polisi.

Alieleza kuwa alishangaa kuiona taarifa hivyo, hivyo akafika hadi Arusha, lakini alishindwa kushiriki katika mkutano huo badala yake alianza safari ya kurudi jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kwenda kwenye Kituo Kikuu cha Polisi Kanda ya Dar es Salaam kwa ajili ya kuripoti.

Akiongozwa na Wakili Peter Kibatala, Gwajima alidai kuwa alifika jijini Dar es Salaam saa 9:30 alasiri ambapo aliunganisha hadi kituoni hapo na kukutana na Ofisa Mpelelezi wa Kanda (ZCO).

Alipoulizwa alikuwa na nani katika safari hiyo, Gwajima alieleza kuwa aliambatana na msaidizi wake Yekonia Bihagaze ambapo alikutana na ZCO wa wakati huo, aliyemtambua kwa jina la Masawe.

Pia alidai kuwa mara ya kukutana na ZCO alimuuliza kama anatafutwa na Jeshi la Polisi ama lah, ndipo ZCO alipomchukua na kumpeleka kwenye chumba kikubwa ambacho kulikuwa na Polisi nane na watu wengine takribani 30.

Alidai kuwa akiwa mkononi amebeba begi lake la kijani alilotoka nalo safari, aliketishwa mbele ya umati huo wa watu kisha kuanza kuhojiwa, hata hivyo wakati mazungumzo yakiendelea kulikuwa na mtu aliyekaa nyuma yake akisoma gazeti ambapo kulikuwa na kitu kikimpalia.

Alieleza kuwa kutokana na hatua hiyo, alianza kupiga kelele kwamba kuna kitu kinamkera ndipo ghafla akajikuta amepoteza fahamu na hakujua nini kilichoendelea.

“Nilipopata fahamu nilijikuta nipo Hospitali ya Polisi Oysterbay ambapo wakati nikiwa kitandani nikamuona mtu aliyevalia mavazi ya Kipolisi ambaye alikuwa na nyota tatu. “Askari huyo alikuja hadi nilipolala na alitaka kunichoma sindano lakini nilikataa na kuanza kubishana naye kwamba mimi nina Daktari wangu katika Hospitali ya TMJ hivyo nipelekwe huko,” alieleza.

Alieleza kuwa wakati akiendelea kubishana na askari huyo ghafla alijikuta akapoteza fahamu na alipozinduka alijikuta yupo Hospitali ya TMJ jijini Dar es Salaam ambapo baadaye alipoteza tena fahamu.

Aidha, alipotakiwa kueleza kama kulikuwa na uwepo wowote wa Polisi katika Hospitali ya TMJ kati ya Machi 27 na 28, alieleza kuwa alimuuliza nesi wa hospitali hiyo ambapo alimwambia ofisini hapo alipekwa na Polisi na wapo nje wanamlinda.

Download App Yetu MPYA  >> BOFYA HAPA << Tukutumie Habari na Burudani Zote FASTA Kila Siku !

No comments

TOA MAONI YAKO HAPO CHINI.