Vita dhidi ya matapeli wa mitandaoni yatangazwa - BongoSwaggz.Com

Advert

Breaking News

Vita dhidi ya matapeli wa mitandaoni yatangazwa

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salam, limetangaza vita dhidi ya matapeli mitandaoni ambao wamekuwa wakitumia jina la mke wa rais mstaafu Salma Kikwete na Mwenyekiti wa IPP, Dk. Reginald Mengi, na kujipatia mamilioni ya fedha kutoka kwa wananchi.

Kamanda wa Kanda hiyo, Kamishna Simon Sirro, alisema matapeli hao wamekuwa wakitumia jina la Salma Kikwete, Dk. Mengi na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, kuwatapeli wananchi.

Alisema wamekuwa wakiwahadaa wananchi watume Sh. milioni moja ili wakopeshwe Sh. milioni 10 na bajaji moja mpya.

Sirro alisema baadhi ya matapeli hao ambao wameshakamatwa, wamekuwa wakifanya utapeli huo kupitia taasisi feki ya ‘Focus Vicoba’ iliyopo kwenye mtandao wa Facebook.

“Kuna uwapo wa taasisi feki ya fedha yenye jina la Focus Vicoba kwenye mtandao wa Facebook na tovuti inayojulikana kwa jina la www.vicobaloanstz.wapka-mob ambayo hutumia majina ya viongozi serikalini na watu maarufu kutapeli,” alisema.

Alisema majina ya viongozi hao yamekuwa yakitumika kufungua akaunti za Facebook na tovuti mbalimbali ambazo matapeli hao hutumia kuwarubuni watu kwamba wanaweza kupata mikopo yenye masharti nafuu na haraka kwa njia ya mtandao.

“Katika ufuatiliaji wa suala hili kitengo cha upelelezi wa makosa ya mtandao cha polisi Kanda Maalumu, kimebaini katika tovuti hiyo picha na jina la Mama Salma limetumika na kwenye ukurasa wa Facebook linatumika jina la Dk. Mengi.

“Wanatumia majina pamoja na namba za simu 0757 308 381 na 0768 199 359 ambazo sio namba za Mama Salma wala Dk. Mengi,” alisema.

Kamanda Sirro alisema ufuatiliaji uliofanyika Desemba 16, mwaka jana uliwezesha kumkamata mtu mmoja (jina tunalo) ambaye kwa sasa ana kesi mahakamani.

Sirro alitoa onyo kwa wale wanaoendelea kufanya udanganyifu na kujipatia fedha kwa njia isiyo halali kupitia mitandao ya kijamii, waache mara moja.

VISHOKA WAPASUA VICHWA POLISI

Kamanda Sirro alisema katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ofisi za Mwenge, lipo kundi linalojihusisha na kazi ya ‘vishoka’ ambalo limekuwa likiwalaghai wateja kwa kuwataka watoe fedha ili kuwasaidia wapate huduma haraka.

“Vishoka hawa wamekuwa wakichukua fomu za wateja kwenye ofisi hizo za TRA na fedha kisha kutokomea nazo,” alisema.

Pia alisema kundi lingine limekuwa likikaa eneo la Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (F.G.B.F) la Askofu Mkuu, Zachary Kakobe lililopo karibu na Mlimani City ambalo limekuwa likichukua fedha za watu kwa kuwadanganya kuwa watawasaidia kuwakutanisha na Kakobe wakati sio kweli.

Kadhalika, alisema kundi lingine limekuwa likiwatapeli watu eneo la Mwenge wanakouza matrekta kwa kuwalaghai wateja kuwa wawape fedha ili kuunganishwa na mmiliki wa biashara hiyo.

Sirro aliwataka wale wote ambao wanatafuta huduma mahali popote wafuate utaratibu uliopo eneo husika na kama wanahisi jambo lolote wawasiliane na jeshi la polisi ama Serikali za Mitaa za eneo husika.

Download App Yetu MPYA  >> BOFYA HAPA << Tukutumie Habari na Burudani Zote FASTA Kila Siku !

No comments

TOA MAONI YAKO HAPO CHINI.