Thamani ya Diamond Platnumz Inayoongozwa na Tamaa - BongoSwaggz.Com

Advert

Breaking News

Thamani ya Diamond Platnumz Inayoongozwa na Tamaa


Diamond anaongozwa na tamaa. Anatamani kufika mahali pakubwa zaidi duniani. Na hiyo ndiyo tofauti kubwa iliyopo kati yake na wanamuziki wengine wa daraja lake Tanzania.

Tamaa ya Diamond inamwelekeza kutumia fedha nyingi kuwekeza. Na uwekezaji huo umekuwa ukimpa matokeo makubwa. Huwezi kummudu Ne-Yo, kumweka Tanzania na kurekodi naye wimbo kisha kufanya naye video Marekani bila uwekezaji.

Kuhusu tamaa bila shaka kila mwanamuziki anayo. Hata hivyo tofauti iliyopo kati ya Diamond na wanamuziki wengine ni jinsi ambavyo anashughulikia tamaa zake kuwa kweli. Anafanya uwekezaji mzuri kupata matokeo anayohitaji.

Kufanya ngoma na P-Square kisha kwenda kuwagharamia kukaa nao Afrika Kusini kurekodi video ya Kidogo, inahitaji uwekezaji.

Tofauti ya Diamond na wanamuziki wengine inaonekana pale kila mmoja anaposhika fedha na kutumia. Diamond hutumia fedha anazopata kuwekeza zaidi kwenye muziki, wakati wengine huzitumbua kwa starehe au kufanya uwekezaji mwingine nje ya muziki.

Wahenga walishatwambia kuwa mtu huvuna anachopanda. Diamond anaonekana ni mwanamuziki mwenye thamani kubwa Tanzania na Afrika yote kwa sasa, sababu ni uwekezaji ambao anaufanya kwenye muziki wake.

Hili ni somo ambalo wanamuziki wengine wanatakiwa kulichukua. Wengi ni wazuri na ubora wao studio ni mkubwa kuliko Diamond. Hata hivyo, Diamond anawashinda kwa ubora nje ya studio.

Narudia kwa msisitizo; Wanamuziki wengi Tanzania ni wazuri na wenye thamani kubwa studio kuliko Diamond. Wanaimba vizuri kuliko Diamond. Hata hivyo, Diamond ana thamani kubwa nje ya studio.

Thamani ya Diamond nje ya studio ni jinsi ambavyo hutafsiri tamaa zake za kufanikiwa kwa kuwekeza ili kupata matokeo anayohitaji. Kupata matokeo kama ya Diamond lazima uwekeze.

Ifahamike kuwa kuwekeza ni kujinyima. Kuna vitu utatamani zaidi lakini utalazimika kuviacha ili kuwekeza katika matokeo makubwa ambayo mtu unakuwa unayaota. Diamond alijinyima kwa ajili kuwekeza ndiyo maana anapata tunayoyaona.

Ndimi Luqman MALOTO

Download App Yetu MPYA  >> BOFYA HAPA << Tukutumie Habari na Burudani Zote FASTA Kila Siku !

No comments

TOA MAONI YAKO HAPO CHINI.