Tambwe aleta faraja Yanga - BongoSwaggz.Com

Advert

Breaking News

Tambwe aleta faraja Yanga

BAADA ya kuwa nje ya timu kwa muda mrefu akiuguza goti, mshambuliaji nyota wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara Yanga, Amissi Tambwe jana alileta faraja kurejea kikosini baada ya kufanya mazoezi na wenzake.

Hata hivyo, nyota huyo alikuwa akifanya mazoezi mepesi 'maalum' kutokana na maelekezo ya daktari wake.

Akizungumza na gazeti hili jana, Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh, alisema kuwa mshambuliaji huyo amerejea kwenye kikosi, lakini uwezekano wa kucheza katika mechi dhidi ya Azam FC itakayofanyika Jumamosi ni mdogo.

Saleh alisema ni faraja kuona nyota huyo anaungana na wenzake hasa wakati huu timu yao ikikabiliwa na mechi ngumu tatu za mashindano mawili tofauti (Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho Afrika).

"Tuna mechi ngumu mbili hapa nyumbani na moja ya marudiano ugenini, tunahitaji kuwa na kikosi imara kitakachohimili ushindani katika mechi hizo tatu zilizo mbele yetu," alisema Saleh.

Tangu ajiunge na Yanga akitokea Simba, mshambuliaji huyo raia wa Burundi alikuwa ni tegemeo, lakini 'makali' yake yamepungua msimu huu kutokana na kuandamwa na maumivu ya goti.

Mechi kati ya Yanga dhidi ya Azam FC ni moja ya michezo itakayoonyesha mwelekeo wa mbio za ubingwa wa Bara ambao unaonekana bado uko wazi.

Timu hizo zitashuka uwanjani zikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare katika mechi ya mzunguko wa kwanza huku Simba ambao ni vinara wao Jumapili wakiwa ugenini Bukoba kucheza na Kagera Sugar.

Mabingwa hao watetezi baada ya kuivaa Azam, wataendelea na mazoezi kwa ajili ya kuwakaribisha MC Alger kutoka Algeria katika mechi ya kwanza ya mtoano kuwania tiketi ya kutinga hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho itakayofanyika Aprili 7, mwaka huu na kurejeana baada ya wiki moja.

Download App Yetu MPYA  >> BOFYA HAPA << Tukutumie Habari na Burudani Zote FASTA Kila Siku !

No comments

TOA MAONI YAKO HAPO CHINI.