Anne Kilango Malecela Asema Haya Baada ya Kuteuliwa Tena Kuwa Mbunge. - BongoSwaggz.Com

Advert

Breaking News

Anne Kilango Malecela Asema Haya Baada ya Kuteuliwa Tena Kuwa Mbunge.

MBUNGE mteule Anne Kilango Malecela amesema ameupokea uteuzi wa ubunge wa Rais John Magufuli juzi, na kusema kuwa Mungu ana sababu za kumrejesha tena katika nafasi hiyo, ambayo ameifanyia kazi kwa muda wa miaka 15.

Uteuzi wa Kilango unazidi kuongeza joto kuwa huenda kukafanyika mabadiliko katika Baraza la Mawaziri, ukizingatia uteuzi uliofanywa na Dk Magufuli wiki iliyopita wa kumteua aliyekuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Wenye Ulemavu), Dk Abdallah Possi kuwa Balozi; pamoja na uteuzi wa wabunge wengine wawili.

Kabla ya Anne Kilango, Dk Magufuli pia alifanya uteuzi wa wabunge wengine wawili, Profesa Palamagamba Kabudi na Abdallah Bulembo kuwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika nafasi zake 10 alizonazo kwa mujibu wa Katiba.

Juzi usiku, Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu ilitangaza kuwa Rais Magufuli amemteua Anne Kilango Malecela kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kwamba ataapishwa kwa mujibu wa taratibu za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza na gazeti hili jana, Kilango alisema anamshukuru Mungu pamoja na Rais Magufuli kwa kuwa na imani naye na kuamua kumteua tena katika nafasi hiyo.

“Kwa kweli sina maneno mengi, namshukuru Mungu na pia ninamshukuru Rais wangu kwa kuwa na imani tena kwangu na kuamua kunipa nafasi hii. Nimekuwa mbunge kwa miaka 15, ni kazi ninayoielewa na ninamuomba Mwenyezi Mungu aniwezeshe ili nifanye kazi itakayowaridhisha,” alisema mbunge huyo wa zamani wa Same Mashariki mkoani Kilimanjaro, ambako alihudumu kwa miaka 15 hadi aliposhindwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Mbunge huyo mteule alisema pia anakwenda bungeni kwa ajili ya serikali, wananchi pamoja na kwenda kukitetea chama chake (Chama Cha Mapinduzi) pamoja na kurekebisha pale panapostahili, lengo likiwa ni kuunga mkono Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dk Magufuli.

“Mungu ana sababu ya kunirejesha tena bungeni. Nitakwenda kufanya kazi nitakitetea chama changu na kukikosoa pale panapostahili pamoja na kuwatetea wananchi wangu na serikali kwa ujumla,” alifafanua Kilango ambaye katika Bunge la Tisa, alijipambanua kuwa mmoja wa wabunge mahiri na kujikita katika kupambana na ufisadi.

Baada ya kushindwa Uchaguzi Mkuu kwa mgombea wa Chadema, mapema mwaka jana, Dk Magufuli alimteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, lakini alidumu katika nafasi hiyo kwa muda wa mwezi mmoja tu, baada ya Rais kutengua uteuzi wake Aprili 11, mwaka jana.

Alitenguliwa nafasi hiyo baada ya kutangaza kwenye vyombo vya habari kuwa mkoa wake hauna watumishi hewa, jambo ambalo lilisababisha Ikulu kufanya uchunguzi wake na kubaini kuwepo kwa watumishi hao, hivyo yeye na Katibu Tawala wake, Abdul Rashid Dachi wakaondolewa katika nyadhifa zao.

“Na wale wote wa Shinyanga ambao walisemekana ni zero, hakuna mtumishi hewa, walikuwa tayari wameshalipwa shilingi milioni 339.9, nimejiuliza sana, na nikajiuliza sana na kwa kweli nimejiuliza sana na kwa masikitiko makubwa, kwa nini Mkuu wa Mkoa alisema hakuna mtumishi hewa?” alisema Dk Magufuli wakati akitangaza kuwavua madaraka Kilango na Dachi.

Kilango ambaye ni mwanamke mpambanaji, mwishoni mwa utawala wa Serikali ya Awamu ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, wadhifa alioushikilia hadi wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Uteuzi wake huo pamoja na wa kina Profesa Kabudi na Bulembo, sanjari na kubadilishiwa kazi kwa Dk Possi, kunazidi kuongeza joto la mabadiliko katika Baraza la Mawaziri, kwani hadi sasa, katika wateule wote wa ubunge wa Dk Magufuli, wamepewa uwaziri ukiondoa mmoja, Naibu Spika Dk Tulia Ackson.

Wabunge wa Kuteuliwa na Dk Magufuli ambao baadaye aliwateua kuwa mawaziri ni Profesa Makame Mnyaa Mbarawa (Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano), Balozi Dk Augustine Mahiga (Mambo ya Nje ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki), Dk Philip Mpango (Fedha na Mipango), Profesa Joyce Ndalichako (Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi) na Dk Possi ambaye sasa amemteua kuwa Balozi.

Kwa uteuzi wa Kilango, Rais Magufuli amefikisha idadi ya wabunge wanane wa kuteuliwa na amebakiza nafasi mbili kwa mujibu wa Katiba. Anne Kilango ni nani?

Alikuwa Mbunge wa Same Mashariki kwa miaka kumi kuanzia 2005 hadi 2015 na alikuwa Mbunge wa Kuteuliwa na Rais kwa miaka mitano kuanzia mwaka 2000 hadi 2005.

Download App Yetu MPYA  >> BOFYA HAPA << Tukutumie Habari na Burudani Zote FASTA Kila Siku !

No comments

TOA MAONI YAKO HAPO CHINI.