Hatma ya Aliyetobolewa Macho na ‘Scorpion’ kwa Mujibu wa Vipimo Kutoka kwa Madaktari. - BongoSwaggz.Com

Advert

Breaking News

Hatma ya Aliyetobolewa Macho na ‘Scorpion’ kwa Mujibu wa Vipimo Kutoka kwa Madaktari.

Vilio vilitawala jana katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam baada ya majibu ya vipimo kutoka kwa madaktari bingwa wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kuonesha kuwa, Said Mrisho (35) aliyetobolewa macho hivi karibuni Buguruni jijini Dar es Salaam, hawezi kuona tena.

Kabla ya majibu hayo, mama mzazi wa Mrisho, Halima Abdallah alikuwa tayari kumtolea jicho moja mwanawe huyo ili kumsaidia aweze kuona tena. Mrisho kabla ya kutobolewa macho alipigwa sehemu mbalimbali za mwili wake na kuchomwa kisu tumboni na Salum Njwele maarufu kama Scorpion, eneo la Buguruni Sheli.

Akizungumza jana, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alisema baada ya kupata taarifa ya tukio hilo waliamua kumpeleka Hospitali ya Muhimbili ili kumfanyia vipimo kuona kama kuna uwezekano wa kuona tena. Alisema alifanyiwa vipimo kwa siku mbili na jopo la madaktari bingwa, lakini majibu yalitoka na kuonesha kuwa hataweza kuona tena.

“Majibu yametoka na ameturuhusu tuyaweke wazi. Majibu ni mabaya ila tumeyapokea inabidi tukubaliane nayo, kwamba ndugu yetu hataweza kuona maisha yake yote,” 
alisema Makonda.

Aliongeza kuwa baada ya majibu hayo Serikali ya Mkoa imejitolea kumpatia matibabu ya kumwekea macho ya bandia ambayo yatamsaidia kurudisha muonekano wa sura yake, kumpatia elimu ya alama ili aweze kuendana na mazingira pamoja na kupatiwa fimbo maalumu.

Pia alisema amepewa gari na dereva kwa ajili ya kumsaidia kwa kipindi chote atakachokuwa kwenye matibabu na mafunzo na atakapofanikiwa ataruhusiwa kuendelea na shughuli zake.

“Tunajua kabla ya kukutwa na majanga haya alikuwa ni kinyozi mzuri, kwa hiyo sisi kama Mkoa tunatafuta kiasi cha Sh milioni 10 kama sehemu ya mtaji wa biashara hivyo amemteua mdogo wake na mke wake kuwa wasimamizi na yeye atakuwa bosi wao,” 
aliongeza Makonda.

Makonda pia aliwataka watu waliobuni mtindo wa kutumia jina la Mrisho kuomba fedha wakijifanya ni yeye, kuacha tabia hiyo kwa vile kitendo hicho hakikubaliki. Kwa upande wake Mrisho, alimshukuru Makonda kwa msaada aliouonesha hadi kufikia hatua hiyo na kusema ameyapokea matokeo hayo, japo hayakuwa mategemeo yake.

“Nimepokea majibu haya kwa majonzi nilijua siku moja nitakufa, lakini sijawahi kuhisi kama nitakuja kutobolewa macho na visu. Aliyefanya kitendo hiki amenitoa mshipa na siwezi tena kuona. Nina majonzi makubwa, lakini sina jinsi sitaweza kuona tena, tukio hili limezima ndoto zangu zote,” alisema.

Aidha, aliwashukuru wote walioonesha msaada kwake katika kipindi chote akiwemo Mkuu wa Mkoa, vyombo vya habari na familia yake.

“Naumia sana ninaposikia mama yangu anataka kunipa jicho lake moja ili nione, lakini najua leo ataumia zaidi. Nawashukuru sana hasa wewe Mkuu wangu wa Mkoa, mke wangu, ndugu zangu na ninyi waandishi wa habari, sina cha kuwalipa,” 
aliongeza.  

-Habari Leo

Download App Yetu MPYA  >> BOFYA HAPA << Tukutumie Habari na Burudani Zote FASTA Kila Siku !

No comments

TOA MAONI YAKO HAPO CHINI.