Ni Muda wa Mashabiki Kuisubiri P-Square Mpya - BongoSwaggz.Com

Advert

Breaking News

Ni Muda wa Mashabiki Kuisubiri P-Square Mpya

Hatimaye maombi na dua za mashabiki wa kundi la P-Square yamekamilika baada ya ujumbe wa Paul Okoye kuonyesha kurudi upya kwa kundi hilo.

Ni muda mrefu umepita tangu kundi hilo linaloundwa na ndugu wawili ambao ni Peter na Paul Okoye kuvunjika na kila mmoja kufanya kazi kivyake. Wakati wa kuvunjika kundi hilo Peter aliachia wimbo wake wa kwanza akiwa mwenyewe ‘Kiss Kiss’ na ‘Look Into My Eyes’ huku akitumia jina la Mr P na Paul alianza kutumia jina la Rude Boy huku akifungua lebo yake iliyokuwa ikiwasimamia wasanii wawili.

Hakika baada ya hatua hiyo muziki wa Nigeria ulionekana kukosa ladha kama tomato unapoikosa kwenye kiepe japo haishibishi hata ukiikosa lakini utatamani kukirudisha kwa muuzaji.

Paul alionekana mara kadhaa kuchukizwa kuvunjika kwa kundi hilo huku akimuomba ndugu yake warudi wafanye kazi kwa pamoja kama zamani lakini kwa wakati huo ilishindikana. “Mpendwa kaka yangu nakuomba, hata kama humtaki tena Jude na hauitaki P-Square, milele utakuwa kaka yangu. Lakini natamani sisi watatu tungeendelea kuwa pamoja sababu ni kitu cha furaha,” aliwahi kuandika Paul Okoye kwenye mtandao wake wa Instagram.

“Watu wanatupenda sana si sababu tu ya muziki wetu mzuri, lakini kuwaona ndugu wakiwa pamoja, kuwa mfano mzuri kwa familia zingine na kwa watoto wetu. Tafadhali, jishushe, samehe na sahau, bado tunaweza kubadilisha hili jambo. Kama nilisema chochote au kufanya chochote nilichokuumiza, nisamehe. Na kwa mashabiki wetu wote wa ukweli, tafadhali tuombeeni. Mungu awabariki wote.”

Hata hivyo mara kadhaa Peter ameonekana kukaa kimya bila kuzungumza chochote huku akiendelea kufanya show peke yake kwa kuzunguka nchi kadhaa ikiwemo Dubai na nchi zingine.

Wimbo wa ‘Kidogo’ wa Diamond ndiyo ulikuwa wimbo wa kwanza wasanii hao ndugu kuonekana mara ya kwanza kwenye video wakiwa pamoja tangu lilipovunjika kundi lao na kuwafanya mashabiki waliowazoea kufurahia kitendo hicho huku wakiwa na matumaini mapya ya kurudi tena kwa kundi hilo.

Mwezi Julai mwaka huu hatimaye aliyekuwa mgumu wa kubadili maamuzi yake, Peter alipost kipande cha video akiahidi kurudi tena na kuwaomba radhi mashabiki wao kwa yaliyotokea lakini pia alitangaza kumrejesha kaka yao, Jude Okoye kama meneja wao. “Something new Cooking in da kitchen and about to come out! From us! You already know it’s P2 baby!!! #KoolestDudes,” aliandika Peter kwenye post yake aliyoiweka kwenye instagram hivi karibuni.
Picha mpya ya Peter na Paul Okoye waliyopiga hivi karibuni.

Hatimaye Paul Okoye ameonekana kufurahia uamuzi huo wa ndugu yake na ameonekana kumsamehe ndugu yake kwa moyo mmoja baada ya hivi karibuni kuweka picha mbili kwenye mtandao wake wa Instagram alizopiga na ndugu yake huyo na kuandika, “History it’s all Good .” “Family is everything ,” aliandika kwenye picha nyingine.

Penye nia pana njia, hakika maombi ya mashabiki hao yanaonekana yameanza kukamilika ni muda wa kusubiri chakula wanachotuandalia huko jikoni.

Download App Yetu MPYA  >> BOFYA HAPA << Tukutumie Habari na Burudani Zote FASTA Kila Siku !

No comments

TOA MAONI YAKO HAPO CHINI.