Simulizi Nzima Kuhusu Kutengana Kwa P Square, Inasikitisha Sana. - BongoSwaggz.Com

Advert

Breaking News

Simulizi Nzima Kuhusu Kutengana Kwa P Square, Inasikitisha Sana.

Habari zilizotikisa katika media mbalimbali kwa miezi kadhaa sasa ni juu ya kutengana kwa washikaji mapacha Peter na Paul Okoye waliokuwa wanaunda Kundi la P Squre.
Upo ubuyu unaodai kwamba jambo lililosababisha mpasuko mkubwa kwenye familia yao ni mke wa Peter, Lola Omotayo kutokana na tofauti zao za Kikabila, kati yake na familia ya mumewe, lakini ubuyu mwingine unadai sababu kubwa ni kaka yao Jude Okoye aliyekuwa msimamizi mkuu wa kazi zao kwa muda mrefu akiwa meneja.

Ukweli ni kwamba hizo ni tetesi tu ambazo zimesambaa kila kona duniani, lakini huu ndiyo ukweli kuhusu kusambaratika kwa kundi hilo kutoka kwa wahusika wenyewe.
MSIKIE MR. PETER
Peter Okoye ambaye ni mkubwa na hafugi rasta, ndiye aliyekuwa wa kwanza kuvujisha taarifa juu ya kutengana kwao miezi kadhaa iliyopita baada ya kuandika kwenye ukurasa wa Twitter ujumbe kuwa si mmoja wa P Square tena!

Akaongeza kuwa amefikia uamuzi huo mgumu baada ya mambo mengi kutokea ambayo binadamu yeyote hawezi kuyavumilia. Baada ya ujumbe huo wa Peter vyombo vingi vya habari vilimtafuta ili kuweza kufungukia ishu nzima. Ambapo akifanya mahojiano na kituo cha habari cha NET, Peter alifunguka kuwa;

“Mpango wa mimi kujitoa P Square ulianza muda mrefu, nimevumilia mambo mengi na jambo ambalo watu wengi hawafahamu, toka Desemba 2015 tulikaa muda mrefu bila kuzungumza na Paul na hiyo ndiyo sababu ya mimi kusafiri mwezi Januari kwenda nje ya nchi maana kichwa changu kilikuwa kinawaza mambo mengi mno.” Anasema Peter na kuendelea kuwa;

Mwaka jana katika Studio ya Mavin, Paul alishirikishwa katika kolabo 4 kwenye ngoma za J- Martins, Bracket, JKT na Gice. Katika video yeye (Peter) japo hakuwa ameshirikishwa kuimba alionekana ili kutengeneza picha ya P Square.

Baada ya hapo yeye pia alishirikishwa kwenye kolabo na Kaha, Darey na Ruggedman. Baada ya kufanya audio kwenye video alimwambia Paul pia alitakiwa kushiriki lakini nduguye huyo alikataa. Jambo lililomuumiza sana.

“Suala hilo liliniumiza, nikamwambia Paul akishiriki katika ngoma yoyote peke yake afahamu hata mimi sitashiriki kwa lolote lile. Tukawa tumekubaliana na baadaye alifanya kolabo na Mr Flavour.

“Nilimtamkia Paul sitashiriki kazi atakayofanya peke yake, lakini alipofanya kolabo na Mr. Flavour alinibembeleza nikakubali. Yalipita, tukaendelea na kazi kwa mawasiliano ya kusuasua, baadaye tulipata mwaliko kwenye sherehe ya binti wa Rais Jonathan Buhari. Katika maandalizi ya mwisho kabisa Paul alidai hatakwenda kushiriki.”

Mr. Peter anasema alifikiri kuwa hayo yalikuwa ni masihara, lakini alikuja kuamini baada ya kufika uwanja wa ndege siku ya tukio akiwa peke yake na akasafiri hadi Abuja pamoja na wacheza shoo pekee.

“Niliumia pia juu ya suala hili, nilijiuliza nitamwambia nini Mheshimiwa Buhari wala sikupata jibu. Nilimshirikisha msaidizi wangu, tulipojadiliana tukakubaliana kudanganya Paul alikuwa mgonjwa.

“Maandalizi yakaendelea tulipokaribia kufanya shoo aliyekuwa meneja wetu, kaka (Jude Okoye) alinipigia simu na kudai yuko uwanja wa ndege (Lagos) anakuja na Paul so tukalazimika kuwasubiri jambo ambalo lilisababisha kuchelewa kufanya onesho letu kiasi kwamba mke wa rais, Patiance Jonathan alikasirika na kutulaumu,” anasema Peter.

Anaendelea kuwa suala hilo nalo likapita. Lakini kitu ambacho kilimvunja kabisa moyo na kuona hakuna uamuzi wa kuendelea kubembeleza juu ya umoja wao ni baada ya Paul kufanya kolabo na Tiwa Savage.

Anasema kuwa walipomaliza kurekodi Tiwa Savage alimtafuta pia Peter na kumwambia alihitaji aingize sauti. Peter anadai Paul alimfanyia figisu huku akimwamba Tiwa, yeye (Peter) hakuwa na uwezo wa kuandika wala kuimba na kazi nyingi za P Square huwa anafanya yeye jambo lililosababisha akasirike mno na kuamua kutangaza kujitoa.
VIPI KUHUSU PAUL?
Tofauti na Jude na Peter, Paul yeye anaonekana kuwa katika majonzi makubwa kutokana na mfarakano wao na katika ‘series’ yote ya sababu za kutofautiana pacha huyo mwenye rasta anaonekana bado anapenda kaka yao Jude kuwa kiongozi wao na bado anahitaji Kundi la P Square kuendelea kuwepo.

Paul japo anashutumiwa na kaka yake kuhusika kwa kiasi kikubwa hadi wao wanatofautiana, baada ya yote kutokea alikuwa kimya na baadaye aliibuka na kibao cha peke yake chenye dakika 1 na sekunde 42 kiitwacho Call Heaven ikiwa ni baada ya saa 24 tu kupita tangu kaka yake Peter atangaze juu ya kufanya kazi akiwa solo.

Katika kibao hicho Paul anaimba kwa majonzi huku katika baadhi ya mistari akilalamika kwa kudai kuwa kama mama yao angekuwa hai hayo yote yasingetokea. Pia anamwambia mama huyo, Josephine Okoye aliyefariki saa tano mbele baada ya kufanyiwa upasuaji wa moyo nchini India, Julai 12, 2012 kuwa atazame duniani namna ambavyo watoto wake wanakoseana.

Mbali na wimbo huo unaosikitisha Paul aliandika pia kwenye ukurasa wa Twitter akimbembeleza kaka yake abadilishe uamuzi aliokuwa ameufikia.

Watu mbalimbali wenye majina makubwa Nigeria wakiwemo wasanii, wanasiasa na hata wafanyabiashara wanasemwa mara kadhaa wamewaweka chini wawili hao na kuwataka wamalize tofauti zao jambo ambalo linaonekana kushindikana.

Hivi karibuni Mr. Peter ametamka wazi kuwapeleka mahakamani ndugu zake Paul na Jude kwa kutumia sura yake kwenye matangazo ya shoo iliyofanyika mapema mwezi huu huko Goma, DR Congo na itakayofanyika Kishasa, DR Congo, Agosti.

Download App Yetu MPYA  >> BOFYA HAPA << Tukutumie Habari na Burudani Zote FASTA Kila Siku !

No comments

TOA MAONI YAKO HAPO CHINI.