Mbinu za Kupata Faida Kubwa Katika Biashara. - BongoSwaggz.Com

Advert

Breaking News

Mbinu za Kupata Faida Kubwa Katika Biashara.

KITU kimoja kizuri kuhusu biashara ambacho wengine hawakipati ni kwamba unapofanya mabadiliko unaweza kuona athari ya yake haraka katika faida. Kama utaanza kuzembea haitachukua muda utaona faida ikishuka na biashara kupata matatizo mengi. Na kama utaanza kuongeza juhudi utaona biashara inakua na faida kuongezeka.

Kipimo kizuri cha juhudi unazoweka katika biashara ni ufanisi wako. Haijalishi ni juhudi kiasi gani unaweka, kama hazileti matokeo chanya basi hazina maana katika biashara yako. Hivyo, kabla ya kusema wewe unaweka juhudi lakini huoni mafanikio, ni vyema ukajiuliza kama juhudi unazoweka zina ufanisi mzuri katika biashara yako?

Juhudi zako zinazalisha ufanisi mzuri pale ambapo unafanya yale muhimu na kuacha kupoteza muda. Pia kutumia vizuri muda unaoupata kuhakikisha unafanya yale majukumu muhimu ya biashara yako.

Changamoto kubwa ambayo kwa sasa tunapitia ni ukosefu wa muda. Muda unaonekana kuwa mdogo kuliko majukumu tunayotaka kutekeleza na kadiri siku zinavyokwenda ndivyo majukumu yanavyoongezeka na muda ni ule ule. Hivyo, bila ya kuwa na mbinu nzuri utajikuta unakimbizana na muda bila ya kuweza kuzalisha kitu chenye faida.

Mbinu muhimu kabisa ya kuongeza ufanisi wako ni kuweza kumiliki muda wako. Inaweza kuonekana rahisi kusema lakini ni kitu ambacho kigumu na chenye changamoto kubwa, hasa kwa dunia ya sasa ambayo ina changamoto nyingi. Wewe kama mfanyabiashara unahitaji kuwa na nidhamu ya muda na nidhamu hii utaipata pale ambapo utaweza kuumiliki muda wako.

Umiliki wa muda unaanza pale ambapo unajua ni yapi majukumu muhimu katika biashara yako, ambayo wewe tu ndio unaweza kuyafanya kwa ufanisi mkubwa. Ndio, kuna majukumu mengi kwenye biashara yako, lakini kuna ambayo wengine wanaweza kufanya. Ni vema ukayaepuka hayo na kuchagua yale ambayo wewe tu ndio unaweza kuyafanya vizuri.

Ukishayajua majukumu haya muhimu kwako, yapangie ratiba ni wakati gani wa siku unayafanya. Na mpango huu unaufanya mapema kabla ya kuianza siku, au kabla ya kulala usiku, kupangilia ya siku inayofuata. Kwa kuwa na ratiba ambayo imeandikwa itakuwa rahisi kwako kuifuata.

Baada ya kujua ratiba yako ya siku ni nini unatakiwa kufanya, ianze siku yako kwa kufanya yale majukumu ambayo ni makubwa na magumu. Hapa ndipo penye changamoto kubwa, kwa sababu majukumu haya makubwa na muhimu huwa yanatisha na ni rahisi kuahirisha na kujiahidi utafanya baadae. Lakini ukishaahirisha na kuianza siku kwa majukumu ambayo si muhimu, hutakuja kurudi tena kwenye majukumu yale ambayo ni makubwa na muhimu.

Jijengee utaratibu wa kwamba kitu cha kwanza kabisa kwenye siku yako ni kutekeleza yale majukumu ambayo ni makubwa na muhimu. Katika wakati huu ambapo unayafanya usikubali usumbufu mwingine wowote. Muda huu utenge na ulinde usije ukapotea. Hakikisha hauanzi siku yako kwa kufuatilia mambo ya kwenye mitandao au kufanya mawasiliano ambayo si muhimu. Kwa sababu ni rahisi kuanza vitu hivi lakini ni vigumu kuacha na unapoacha unajikuta huna tena nguvu ya kuendelea na majukumu mengine muhimu.

Mwanzo wa siku, yaani asubuhi ni wakati mzuri sana wa kutekeleza majukumu makubwa na muhimu. Hii ni kwa sababu kwa watu wengi asubuhi bado wanakuwa na nguvu na akili zinafanya kazi bila ya uchovu. Lakini kadiri siku inavyokwenda nguvu inapungua na akili inachoka. Ndio maana mwishowe unakuwa umechoka na huwezi kufanya uamuzi mkubwa kwa usahihi.

Mbinu bora kabisa ya kuongeza ufanisi wako kwenye biashara ni kujua yale majukumu muhimu ambayo wewe tu ndiye unayeweza kuyafanya na kuyafanya asubuhi na mapema kabla ya kuendelea na majukumu mengine ambayo si makubwa, pia si muhimu.

-Mtanzania

Download App Yetu MPYA  >> BOFYA HAPA << Tukutumie Habari na Burudani Zote FASTA Kila Siku !

No comments

TOA MAONI YAKO HAPO CHINI.