Kilo 132,975 za Sukari Zagawiwa Bure - BongoSwaggz.Com

Advert

Breaking News

Kilo 132,975 za Sukari Zagawiwa Bure

Dar/mikoani. Wakati sukari ikiendelea kuadimika na kupanda bei, Mamlaka ya mapato TRA mkoani Lindi imetaifisha na kugawa bure kilo 132,975 za sukari kwa taasisi 31 za umma.

Sukari hiyo yenye thamani ya Sh373,521,618 imegawiwa kwa kambi za wazee, shule maalumu, hospitali, shule za kawaida, magereza na vyuo mbalimbali baada ya kuthibitishwa na Mamlaka ya chakula na dawa (TFDA) kuwa salama kwa matumizi ya binadamu.

Sukari hiyo ya Brazil iliwekwa kwenye mifuko 5,319 yenye ujazo wa kilo 25 kila mmoja, ilikamatwa Februari katika bandari ya Lindi, ilipokuwa ikiingizwa nchini kinyume na sheria pamoja na mafuta ya kula ambayo hayakuwa salama kwa matumizi ya binadamu.

Akizungumza wakati wa ugawaji wa sukari hiyo, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi, Richard Kayombo alisema baada ya kukamatwa kwa bidhaa hizo, TRA kwa kushirikiana na taasisi nyinginezo za Serikali iliamua kuigawa sukari hiyo kwa watu wenye mahitaji kwa wilaya zote za mkoa wa Lindi.

“Februari Mosi, mwaka huu mamlaka ya mapato kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama tulikamata meli ya Mv Asant iliyokuwa inaongozwa na Abdushir Swalehe ikitokea Zanzibar, ilikuwa imebeba shehena ya sukari na bidhaa zingine zilizoingia nchini kinyume na taratibu,” alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Yahaya Nawanda kwa niaba ya mkuu wa mkoa, alizitaka taasisi zote zilizopata sukari hiyo kuzitumia kama ilivyoelekezwa na hairuhusiwi kuiuzwa popote.

Aliwasihi wafanyabiashara kufuata taratibu za nchi na kujiepusha na biashara za kimagendo, kwani mkoa huo umejipanga kupambana nao.

Bei yazidi kupaa

Kwa sasa sukari katika maeneo mbalimbali nchini inauzwa kati ya Sh2,600 hadi 4,000, licha ya Rais Magufuli kuwataka wafanyabiashara kutokuificha na kupunguza bei yake.

Jijini Mwanza katika kata za Igogo, Pamba, Mahina, Mbugani, Mabatini, Mkuyuni, Nyegezi, Butimba kilo moja ya sukari jana ilikuwa inauzwa Sh4, 000 huku baadhi ya maduka ya rejareja yakisitisha kutoa huduma hiyo. “Hii ina inaleta picha gani? Kila Rais anaposema kupunguza bei, ndipo inazidi kupaa mara dufu,” alihoji Juma Masanja mkazi wa Bugarika.

Kaimu Kamanda wa polisi wa mkoani Mwanza, Augustino Senga alisema polisi inaendelea na ukaguzi wa maghala, ili kuwabaini wafanyabiashara wanaoficha sukari makusudi.

Kutoka Bukombe, Ofisa Biashara wilaya hiyo, Celestin Mwamba amewataka wananchi kuisaidia Serikali pindi watakapobaini ukiukwaji wa agizo la uuzwaji wa sukari zaidi ya bei elekezi ya Sh1, 800 kwa kilo.

Download App Yetu MPYA  >> BOFYA HAPA << Tukutumie Habari na Burudani Zote FASTA Kila Siku !

No comments

TOA MAONI YAKO HAPO CHINI.