Rais Magufuli Ahamishia Utumbuaji Majipu EAC - BongoSwaggz.Com

Advert

Breaking News

Rais Magufuli Ahamishia Utumbuaji Majipu EAC

Bet Sasa
Rais John Magufuli akiwa na Rais wa Uganda Yoweri Museveni

Mwenyekiti mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Rais Dk. John Magufuli, ametangaza rasmi kutumbua majipu yote atakayokuta katika Sekretarieti ya jumuiya hiyo.

Pia amepiga marufuku Sekretarieti hiyo kuwa na mipango yenye gharama kubwa kwa EAC, huku akitoa mfano wa Hoteli ya Ngurdoto ulikofanyika mkutano huo jana kuwa ni sehemu ya matumizi hayo mabaya ya fedha ambayo hapendi kushuhudia..

Akitumia kauli mbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’ katika mkutano huo kuwa majipu yote atakayoyabaini ambao si Watanzania, ataripoti kwa viongozi wao ili wachukuliwe hatua na mamlaka zao.

Mkutano huo ulihudhuriwa na Marais wa Rwanda, Paul Kagame, Uganda, Yoweri Museveni, Kenya, Uhuru Kenyatta, wakati Burundi alihudhuria Makamu wa Rais na kutoka Sudani Kusini alikuja Makamu wa Pili wa Rais, James Wahadi.

Akifunga mkutano huo ulioanza majira ya saa 8:15 mchana hadi saa 11:20 jioni, Dk Magufuli alisema nchi wanachama wa jumuiya hiyo ni maskini hivyo kuna umuhimu wa kubana matumizi.

Alisema kwa mfano, gharama ya kwa kila mshiriki wa mkutano huo wa jana ni Dola za Marekani 45 kiasi ambacho ni kikubwa la laiti mkutano huo ungefanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Arusha, gharama yake ingekuwa chini ya hapo.
Rais John Magufuli akiwa na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta

Alisema kila nchi mwanachama ina matatizo yake hiyo suala muhimu hapo ni kuvumiliana ili jumuiya hiyo iweze kusonga mbele.

Mapema katika hotuba yake, alisema wakuu hao wamemchagua kuwa Mwenyekiti wa jumuiya hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Kuchaguliwa kwake kunaifanya Tanzania kuwa Mwenyekiti wa jumuiya hiyo kwa awamu mbili sasa.

Rais mstaafu Jakaya Kikwete, alikuwa Mwenyekiti wa jumuiya hiyo kwa kuongoza kwa miezi minane kabla ya kumwachia Dk. Magufuli ambaye ameongoza kwa kipindi cha miezi minne.

Akizungumzia suala la amani nchini Burundi, alisema wakuu hao kwa pamoja wamekubalina kuharakisha kutafuta amani ya nchi hiyo.

Alisema katika kufanikisha suala hilo, wakuu hao wamemchagua Rais mstaafu Benjamin Mkapa, kuwa msuluhishi wa mgogoro wa Burundi kazi ambayo atakuwa akiifanya chini ya Rais wa Uganda, Yoweri Museveni ambaye alikwishaianza.

Alisema nchi zote zimekubaliana kuharakisha suala la kupata amani ya Burundi na kwa kutumia dhana ya Hapa Kazi Tu, amani nchini humo itapatikana haraka.

Alisema wakuu hao pia wamekubali kuipokea nchi ya Sudani Kusini kuwa mwanachama mpya wa EAC, huku akimtangaza Liberat Mfumukeko kutoka Burundi kuwa Katibu Mkuu mpya aliyechaguliwa na viongozi hao.

Kuhusu matumizi ya lugha katika shughuli mbalimbali za jumuiya hiyo, alisema ni wakati muafaka sasa kutumia lugha ya Kiswahili kwani hata Umoja wa Afrika umeifanya lugha hiyo kuwa rasmi katika shughuli zake.

Kwa upande wa viwanda, alizitaka nchi wanachama kuweka mikakati ya ujenzi wa viwanda vya nguo na ngozi kwani ni muhimu kwa kuwa ina soko kubwa la watu zaidi ya milioni 145.
Rais John Magufuli akiwa na Rais wa Rwanda Paul Kagame

“Lazima tuwe na mikakati ya kuwa na viwanda na tutumie kile tunachozalisha,” alisema.

Kuhusu utoaji wa mizigo bandarini, alisema hali sasa imeboreshwa kwa upande wa Tanzania ambapo hutumia siku tatu tu kutoa mzigo bandarini na kuusafirisha hadi Kigali nchini Rwanda badala ya siku 20 za awali.

Kwa upande wa Kenya, alisema, wanatumia siku nne kutoa mzigo bandari ya Mombasa hadi Uganda badala ya siku 18 za awali huku kusafirisha mizigo hiyo kutoka bandari hiyo hadi Kigali hutumia siku sita badala ya 21 za awali.

Mapema Katibu Mkuu wa EAC anayemaliza muda wake, Dk Richard Sezibera, alisema anamaliza akiwa amefanikisha masuala mengi muhimu aliyepewa kuyafanya katika uongozi wake.

Aliyataja baadhi ya masuala hayo kuwa ni soko la pamoja, mtangamano wa EAC, mchakato wa sarafu moja na miundombinu.

Katika mkutano huo viongozi hao walizindua hati ya kimataifa ya kielektroniki ya kusafiria ya nchi za Afrika Mashariki na pia
walizindua mwongozo wa kanuni za biashara utakaotumika kwa nchi za Afrika Mashariki.

Pia Dk. Magufuli aliwatunuku vyeti na fedha wanafunzi watano walioshinda kuandika isha.

Aliyeshinda nafasi ya kwanza ni Simon Sabaya Mollel mwanafunzi aliyemaliza kidato cha nne Shule ya Sekondari Mzumbe, Tanzania alipata dola za Marekani 1500 huku nafasi ya pili ikishikwa na Mungai Beryl alipata dola 1200 kutoka Kenya.

Mwanafunzi aliyeshika nafasi ya tatu ni Iteka Greta kutoka Rwanda aliyepata dola 1000 huku nafasi ya nne ikishikwa na Azookire Oscar kutoka Uganda alipata dola 750 na nafasi ya tano ilikwenda kwa Irumvya Alley kutoka Burundi aliyepata dola za Marekani 650.

Chanzo: NIPASHE

Download App Yetu MPYA  >> BOFYA HAPA << Tukutumie Habari na Burudani Zote FASTA Kila Siku !

No comments

TOA MAONI YAKO HAPO CHINI.