Maalim Seif Awatoa Hofu Wazanzibari..Ni Baada ya maneno ya Kizushi. - BongoSwaggz.Com

Advert

Breaking News

Maalim Seif Awatoa Hofu Wazanzibari..Ni Baada ya maneno ya Kizushi.

ALIYEKUWA mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amewatoa hofu Wazanzibari kuwa bado yupo hai na afya yake imeimarika.

Ametoa kauli hiyo Dar es Salaam jana, baada ya taarifa kusambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa yuko mahututi, huku mingine ikidai amefariki dunia.

Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa chama hicho, alizidiwa ghafla juzi akiwa kwenye ndege wakati akitoka Zanzibar kwenda Dar es Salaam.

Uvumi huo umekuja zikiwa zimebaki siku 10 kabla ya kufanyika uchaguzi wa marudio visiwani Zanzibar, baada ya ule wa awali kufutwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), mwaka jana.

Kuenea kwa uvumi huo kulisababisha vyombo vya habari kutafuta ukweli katika Hospitali ya Hindu Mandal, Dar es Salaam alikokuwa amelazwa kiongozi huyo.

Ilipofika saa 7:00 mchana, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa CUF, Ismail Jussa akiwa na viongozi wengine mbalimbali wa chama hicho, aliwaambia waandishi wa habari kuwa Maalim Seif ni mzima wa afya.

Dakika 20 baadaye, Maalim Seif alitoka wodini alikokuwa amelazwa kwa kutumia ‘lifti’ akiwa ameambatana na daktari wake na watumishi wengine wa hospitali hiyo na kuanza kuwapungia mkono wananchi waliokuwa wakisubiri matibabu.

“Alhamdulilah, namshukuru Mungu mimi sijambo, ni mzima kabisa,” alisema huku akitembea mwenyewe bila msaada wa mtu akiwafuata wanahabari.

Akisimulia kilichotokea hadi akafikishwa hospitalini hapo na kulazwa, Maalim Seif alisema kuwa akiwa Uwanja wa Ndege wa Zanzibar kuja Dar es Salaam juzi, ghafla alisikia kizunguzungu.

“Namshukuru Mungu nilikwenda bara Hindi (India) kwa matibabu ambako nilifanyiwa upasuaji wa uti wa mgongo na Ijumaa ya wiki iliyopita nilirudi salama na nikapokewa vizuri Zanzibar.

“Nikapumzika Jumamosi na Jumapili, siku ya Jumatatu nikaja Dar es Salaam, nimeondoka nyumbani mzima kabisa, bahati mbaya kufika ‘airport’ ghafla nikajisikia kizunguzungu, ikabidi wenzangu wanisaidie kupanda kwenye ndege,

“Tulifika Dar es Salaam salama, nikaletwa na kulazwa hapa Hindu Mandal na wenzetu walikuwa wamejiandaa vizuri, wakaanza kunifanyia vipimo,” alisema.

Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar iliyomaliza muda wake tangu Oktoba, mwaka jana, alisema madaktari walichukua vipimo na kuvifanyia uchunguzi.

Alisema akiwa anaendelea kupatiwa matibabu, baada ya saa mbili kupita hali yake ilirejea kama kawaida.

“Watanzania wasiwe na wasiwasi, mimi ni mzima, nimelala vizuri, nimeamka salama asubuhi, nimefanya mazoezi na naweza kutembea mwenyewe, hali yangu ni nzuri na hata mtu akitaka tushindane kutembea hadi Kibaha naweza,” alisema na kusababisha kicheko kwa wenzake.

Alisema kuwa anawashukuru wananchi, Wazanzibari, Watanzania wa ndani na nje ya nchi ambao wameonyesha mapenzi makubwa kwake.

“Wengi walikuwa na wasiwasi na wengine waliposikia nimeumwa kiasi hicho walizirai na kupoteza fahamu, yote hiyo ni dalili wananchi wana mahaba na mimi, nami nawapenda sana,” alisema huku akisisitiza kauli aliyoambiwa na madaktari wake kwamba angeweza kupata ruhusa ya kurejea nyumbani wakati wowote jana.

Download App Yetu MPYA  >> BOFYA HAPA << Tukutumie Habari na Burudani Zote FASTA Kila Siku !

No comments

TOA MAONI YAKO HAPO CHINI.