Kikwete: Nitaachia uenyekiti, lakini sitaacha vikao vya ndani CCM - BongoSwaggz.Com

Advert

Breaking News

Kikwete: Nitaachia uenyekiti, lakini sitaacha vikao vya ndani CCM


Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dk. Jakaya Mrisho Kikwete (katikati), Kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara) Ndugu Philipo Mangula na Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahman Kinana (kulia)

Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete amesema hata akimkabidhi Rais John Magufuli uenyekiti wa CCM, bado ataendelea kushiriki vikao vya ndani vya chama hicho.

Kwa mujibu wa utaratibu wa CCM, Rais ndiye anakuwa mwenyekiti wa chama katika uchaguzi unaofuata baada ya Uchaguzi Mkuu. Hata hivyo, mwenyekiti aliyeachia urais, amekuwa akiachia pia uenyekiti wa CCM hata kabla ya muda wa kikatiba wa uchaguzi wa viongozi wa chama kufika.

Uchaguzi wa viongozi wa CCM unatakiwa kufanyika mwaka 2017, lakini tayari Kikwete ameshaeleza kuwa ataachia uenyekiti mapema.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa kitabu cha maisha ya Kepteni John Komba uliokwenda sambamba na kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu kufariki kwa muasisi huyo wa kikundi cha burudani cha TOT , Kikwete alisema ataendelea kuchangia mawazo na mapendekezo yake kutokana na uzoefu wake katika nafasi hiyo.

“Uenyekiti wa Chama cha Mapinduzi nitaachia, lakini mambo ya ndani yanayohusu chama hiki sitaacha kushiriki,” alisema Kikwete.

Akimzungumzia marehemu Komba, Kikwete alisema alifahamiana naye kwa muda mrefu na kuwa walistaafu wakati mmoja jeshini.

Katika uzinduzi wa kitabu hicho kilichopewa jina la Maisha ya Mzalendo John Komba, Kikwete aliahidi kuanzisha harambee kwa ajili ya kukinadi kitabu hicho ambacho fedha zitakazopatikana zitatumika katika ujenzi wa shule mbili zilizoanzishwa na Kapteni Komba, moja itapewa jina la Kapteni Komba na nyingine Colleta.

Komba aliongoza kikundi cha sanaa cha CCM kinachoitwa Tanzania One Theatre (TOT) alichokianzisha akitokea jeshini mara baada nchi kuruhusu siasa za ushindani mwaka 1992.

Kitabu hicho chenye kurasa 58 kinachoeleza maisha ya Komba na kilichoandikwa na Yusuf Halimoja, kitauzwa Sh10,000 na nakala 5,000 zitasambazwa mikoa yote kwa ajili ya kutafuta fedha za kujenga shule ya kumbukumbu ya Komba.

Akisoma risala, Salome ambaye ni mke wa kiongozi huyo wa zamani wa kundi la TOT, alisema Komba aliandika wosia wake kwa mkono wake ndio maana familia haikupata shida mpaka sasa.

Salome, ambaye kwa taalumu ni mwalimu, alisema licha ya mumewe kuwa na shinikizo la damu kwa kipindi cha miaka kumi na baadaye kugundulika kuwa na ugonjwa wa kisukari, lakini deni la benki ya CRDB lilichangia kifo chake.

Alisema alipokea simu kutoka CRDB ikitoa siku saba wawe wametoa vitu katika shule za Bakili Muluzi na Colleta na baada ya kumtaarifu mumewe, alifariki siku chache baadaye.

Chanzo: Mwananchi

Download App Yetu MPYA  >> BOFYA HAPA << Tukutumie Habari na Burudani Zote FASTA Kila Siku !

No comments

TOA MAONI YAKO HAPO CHINI.