Rais Kikwete Ahadharisha Jeshi la Polisi - BongoSwaggz.Com

Advert

Breaking News

Rais Kikwete Ahadharisha Jeshi la Polisi

Zikiwa zimesalia siku nne Uchaguzi Mkuu ufanyike, Rais Jakaya Kikwete amelitaka Jeshi la Polisi nchini kuwa makini na watu aliowataja kuwa chanzo cha kuleta vurugu siku ya kupiga kura, Jumapili hii.
Rais Kikwete ambaye alilipongeza pia jeshi hilo kwa kusimamia vizuri mikutano yote ya kampeni tangu ilipoanza, alisema mtihani uliobakia sasa ni wa kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa amani na usalama.
Kauli hiyo aliitoa jana katika Viwanja vya Chuo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, baada ya kupokea magari 399 yatakayotumiwa na jeshi hilo.
Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, magari hayo ni kati ya 777 yaliyonunuliwa na Serikali kutoka India.
“Mmesimamia vizuri mikutano ya kampeni, ninawapongeza, lakini msionyeshe ulegevu kwenye hatua ya mwisho iliyo mbele yenu, hakikisheni mnawazuia wote wanaotaka kuleta vurugu na kuwafanya watu waogope kwenda kupiga kura,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Lakini sijasema muwaonee watu, badala yake hakikisheni mnakuwa wakali kwa wote watakaoonyesha dalili za kuvunja sheria. Tunachotaka watu wapige kura wakiwa katika hali ya utulivu bila hofu.”
Miongoni mwa magari aliyoyapokea ni malori maalumu kwa ajili ya kazi ya kubebea askari, magari ya Zimamoto na mengine manane maarufu washawasha kwa ajili ya kuzuia vurugu.
Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe alitumia nafasi hiyo kukanusha uvumi ulioenea mitaani kuwa magari hayo yameletwa kwa ajili ya kutumika katika kipindi hiki cha uchaguzi.
“Uvumi huo hauna ukweli, magari haya tumeyaleta kwa ajili ya kuliongezea ufanisi wa kazi jeshi letu la polisi ambalo kwa muda mrefu limepungukiwa vitendea kazi yakiwamo magari,” alisema Chikawe.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Rais Kikwete aliyesema:
“Maneno ni mengi na watu wamezoea kusema, lakini ukweli unabakia kuwa magari haya yamenunuliwa kwa ajili ya kuongeza ufanisi wa kazi ndani ya jeshi letu.”
Wakati huohuo; Rais Kikwete alisema anaondoka madarakani akiliacha jeshi hilo likiwa salama na imara licha ya kutokamilisha baadhi ya mahitaji yake aliyoahidi kulipatia.
“Naondoka jeshi likiwa imara, lakini kuna vitu havijakamilika ila tayari kuna fedha zimeshatengwa kwa ajili hiyo,” alisema Rais Kikwete.

-mwananchi

Download App Yetu MPYA  >> BOFYA HAPA << Tukutumie Habari na Burudani Zote FASTA Kila Siku !

No comments

TOA MAONI YAKO HAPO CHINI.