NEC: Chadema Inatupa Shida - BongoSwaggz.Com

Advert

Breaking News

NEC: Chadema Inatupa ShidaMwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu, Damian Lubuva
Dar/Arusha. Ombi la Chadema la kutaka wataalamu wa Tehama wa vyama vya siasa na waangalizi wa kimataifa waruhusiwe kukagua programu itakayotumika kuhesabu kura za urais, limesababisha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kukitaja chama hicho kuwa ndicho pekee kinachoipa shida katika utekelezaji wa majukumu yake.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu, Damian Lubuva ambaye hata hivyo alisema Tume yake itakutana na wawakilishi wa vyama vyote muda mfupi kabla ya siku ya upigaji kura ili watoe madukuduku waliyonayo.
“Tunasubiri walete hilo ombi. Lakini hata wasipofanya hivyo tutakuwa na kikao na vyama vyote vya siasa baada ya kumalizana na wadau wengine.
“Chadema wana wasiwasi mwingi na ndicho chama kinachotupa shida mara nyingi. Tukifanya hivi, wao wanataka hivi,” alisema Jaji Lubuva alipokuwa akijibu maombi ya Chadema yaliyotolewa jana na Naibu Katibu Mkuu wake, John Mnyika alipozungumza na vyombo vya habari.
Mnyika aliitaka NEC kuruhusu wataalamu wa Tehama wa vyama vya siasa na waangalizi wa kimataifa nao waende NEC na wataalamu wao kuhakiki mfumo utakaotumika kupokelea kura za urais kwa lengo la kujua kama uko salama ili kuzuia uchakachuaji wa matokeo.
Mnyika alidai kuwa kuna mazingira ya kupigwa ‘bao la mkono’ yanayotengenezwa na ndiyo maana ni muhimu mambo yote yakawekwa wazi ili kuzuia uchakachuaji wa matokeo.
“Lubuva akubali kuanzia sasa tuchambue huo mfumo na wataalamu wetu waukague ili wajue kama uko salama usije ukawa ni wa kuiba kura na kutupiga ‘bao la mkono’,” alisema Mnyika.
Mbali na hilo, Mnyika alidai kuwa anashangaa kwa nini NEC hadi sasa haijawasilisha daftari la awali la wapigakura kwa vyama vya siasa ili walihakiki.
“Kwa nini hadi sasa hawajatukabidhi daftari, lazima tupewe kama ilivyofanyika mwaka 2010,” alisema Mnyika na kuongeza: “Suala la kwamba NEC inasema uhakiki umefungwa wakati sisi hatujakabidhiwa hilo daftari kulihakiki, kuna mazingira ya bao la mapema la mkono.”
Mnyika alisema mwaka 2010, daftari hilo lilivisaidia vyama vya siasa kuwaonyesha wananchi ambao walikosa majina yao vituoni kuwaelekeza vituo vyao kutokana na majina kuwapo kwenye daftari lakini yakikosekana kwenye orodha zinazobandikwa vituoni.
“Daftari hili ni muhimu sana, mwaka 2010 tuliweka dawati letu kwenye vituo. Wananchi ambao walifika kituoni na kukosa majina yao kwenye orodha iliyobandikwa tuliwaambia waende kwenye dawati la Chadema waangaliziwe kwenye daftari na walipokuta majina yapo tuliwaambia wapige kura na walifanya hivyo bila matatizo,” alisema Mnyika.
Aliwataka wananchi kuwa makini na suala hilo na kuhakikisha wanapiga na kulinda kura ili kuzuia uchakachuaji wa matokeo.
Pamoja na kwamba Jaji Lubuva alisema matokeo yote yatabandikwa vituoni, hivyo wananchi wapige kura na kuondoka, Mnyika alipinga na kuwataka wananchi kutomsikiliza kwani kuondoka vituoni kunatoa mazingira ya kuibwa kura.
Hata hivyo, Mnyika alisema pamoja na mazingira mbalimbali ya bao la mkono yanayotengenezwa, mwaka huu ni wa mabadiliko, hivyo wana Ukawa wasikate tamaa.
“Kuna matumizi mabaya ya rasilimali za Serikali, lakini tunasema wamtumie rais, watumie mawaziri, mwaka huu ni wa mabadiliko,” alisema Mnyika.
Polisi hawatoshi vituo vya uchaguzi
Katika hatua nyingine; NEC imesema kutokana na uhaba wa askari polisi, watu wengine watakaoidhinishwa na jeshi hilo wataongeza ulinzi pale patakapopungua.
Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Emmanuel Kawishe alisema hayo jana katika mkutano kati ya Tume hiyo na Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (Moat) ambao ulijadili mwenendo wa mchakato huo na changamoto zilizopo kuelekea Oktoba 25.
“Ninatambua changamoto iliyopo kwa Jeshi la Polisi ambalo lina askari 43,000 ilhali vituo vilivyotangazwa ni 72,000. Watu watakaotakiwa kujaza nafasi hizo watalazimika kuthibitishwa na jeshi hilo kabla hawajatekeleza majukumu watakayopangiwa,” alisema Kawishe.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Ernest Mangu alisema ni la kawaida na kila wakati wa uchaguzi huwa wanafanya hivyo.
Kituo cha wazi majumuisho
Wakati Chadema ikisema hayo, Mhadhiri Mwandamizi wa Kitivo cha Sheria, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk James Jesse ameishauri NEC kuandaa kituo cha wazi cha majumuisho ya kura za urais ambacho kitakuwa kikipokea matokeo kwa uwazi na kuyajumlisha ili kuondoa usiri ambao unaweza kusababisha vurugu baada ya uchaguzi.
Dk Jesse alitoa ushauri huo katika mkutano wa Kamati ya Amani Arusha (Apet) inayojumuisha viongozi wa siasa, dini, polisi na wa Serikali ili kujadili masuala mbalimbali kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Alisema nchi mbalimbali zimekuwa na utaratibu wa kuwa na kituo kimoja ambacho kinaonyesha kwa uwazi kura zinapofikishwa kutoka kwenye majimbo na kujumlishwa ili kuondoa hofu ya vurugu baada ya matokeo.
“Tumeona uchaguzi ambao jambo hili linafanyika, hata katika nchi za Afrika kama Ghana nadhani ni utaratibu mzuri kuondoa malalamiko yasiyo na sababu,” alisema.
Katibu wa Bakwata Mkoa wa Arusha, Juma Masoud na Mchungaji Simon Irunde walisema kamati hiyo, imejipanga kutoa elimu ili kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa huru na haki.

Moat

Mwenyekiti wa Moat, Reginald Mengi aliitaka NEC kuongeza nguvu kwenye elimu ya mpigakura ili kuwaandaa wananchi wengi zaidi kushiriki kikamilifu huku akihimiza wagombea na viongozi wa vyama kuzingatia maadili ya uchaguzi.

Mjumbe wa NEC, Profesa Amon Chaligha alisema wananchi wa kila eneo, wanapaswa kujua nani ameshinda kutokana na kura zao na hilo litapatikana kutoka katika vyombo vya habari.
Alisema msimamo wa Tume ni kuwaruhusu waandishi wa habari kutembelea vituo vya uchaguzi ili kujionea mwenendo wa upigaji kura na kuchukua matokeo yatakayobandikwa na ikiwezekana kuwahoji wasimamizi au wapigakura watakaokuwapo kwenye vituo husika.
“Vyombo vya habari vinaruhusiwa kutangaza matokeo yote yaliyotangazwa kwenye vituo kwa manufaa ya wananchi wa eneo husika. Kitu pekee wasichotakiwa kufanya ni kumtangaza mshindi au kutaja jina la yeyote mwenye uwezekano wa kushinda kwa kutumia matokeo waliyonayo,” alisema Profesa Chaligha.

Usajili wa waandishi

Ili kurahisisha upataji wa habari kutoka kwa wasimamizi, waangalizi na wapigakura, NEC imeandaa vitambulisho maalumu vitakavyotumika na tayari wanahabari 311 wa ndani na kumi na moja wa kimataifa wametuma maombi.
Kamishna wa Tume hiyo, Jaji mstaafu, John Mkwawa alisema maombi ya wanahabari wote yanaratibiwa na Idara ya Habari (Maelezo).

Imeandikwa na Boniface Meena, Mussa Juma na Julius Mathias.

-Mwananchi

Download App Yetu MPYA  >> BOFYA HAPA << Tukutumie Habari na Burudani Zote FASTA Kila Siku !

No comments

TOA MAONI YAKO HAPO CHINI.