‘Kikwete Kuongoza Hadi Raisi Mteule Atakapoapishwa’ - BongoSwaggz.Com

Advert

Breaking News

‘Kikwete Kuongoza Hadi Raisi Mteule Atakapoapishwa’

Serikali imesema Rais Jakaya Kikwete na baraza lake la mawaziri wataendelea kufanya kazi hadi rais mteule atakayeshinda katika Uchaguzi Mkuu atakapoapishwa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, Serikali imetoa ufafanuzi huo baada ya kuwapo kwa mijadala kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari, kuhusu ukomo wa madaraka ya rais na mwisho wa Baraza la Mawaziri.
Katika taarifa hiyo, Sefue alisema kwa mujibu wa Katiba, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ataendelea kushikilia nafasi hiyo akiwa na mamlaka yote yanayoambatana na nafasi hiyo, hadi rais mteule atakapoapishwa.
“ Ibara ya 42(3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, inasema ukiacha sababu nyingine, mtu anayechaguliwa kuwa rais atashika madaraka ya kiti hicho hadi rais mteule atakapoapishwa,” alisema Sefue.
Aliwataka wananchi waelewe kuwa hakutatokea wakati ambao rais na Amiri Jeshi Mkuu mwenye mamlaka kamili, atakayekuwa tayari kutelekeza mamlaka yake.
“Lengo ni kuhakikisha kuwa haitokei wakati wowote nchi yetu ikakosa Rais na Amiri Jeshi Mkuu,” alisema.
Alisisitiza kuwa madaraka na mamlaka ya rais yapo, na hayapungui kwa namna yoyote ile, hata baada ya Uchaguzi Mkuu, kabla ya kuapishwa kwa rais mpya, mpaka Rais Mteule atakapoapishwa.
Kuhusu ukomo wa Baraza la Mawaziri, Sefue alisema katika taarifa hiyo kuwa yataendelea mpaka rais mteule atakapokula kiapo.
“Kwa mujibu wa Ibara ya 57(2) ya Katiba, Waziri na Naibu Waziri ataendelea kushikilia mamlaka ya nafasi yake hadi, ukiacha sababu nyingine hadi rais mteule atakapoapishwa,” alisema.
Alisema Mawaziri na Naibu Mawaziri wataendelea kushikilia nafasi zao, wakiwa na madaraka na mamlaka kamili yanayoambatana na nyadhifa zao.
Sefue alivitaka vyombo vya habari kusaidia kuwaelimisha wananchi kuhusu utaratibu wa kubadilishana madaraka kati ya awamu moja ya uongozi wa nchi na nyingine.
“Madaraka na mamlaka ya Rais yapo hayapungui kwa namna yoyote ile, hata baada ya uchaguzi Mkuu mpaka Rais Mteule atakapoapishwa,”alisema.

Chanzo - Mwananchi

Download App Yetu MPYA  >> BOFYA HAPA << Tukutumie Habari na Burudani Zote FASTA Kila Siku !

No comments

TOA MAONI YAKO HAPO CHINI.