SIASA: Lowassa Aahidi Kufumua Mikataba ya Gesi na Mafuta...Sumaye Amtaka Magufuli Ahamie UKAWA - BongoSwaggz.Com

Advert

Breaking News

SIASA: Lowassa Aahidi Kufumua Mikataba ya Gesi na Mafuta...Sumaye Amtaka Magufuli Ahamie UKAWA

Mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, amesema akichaguliwa na kuingia madarakani baada ya uchaguzi mkuu Oktoba 25, atahakikisha kuwa mikataba yote ya gesi na mafuta inapitiwa upya ili kuhakikisha kuwa kweli inawanufaisha Watanzania na siyo wawekezaji wa kigeni peke yao.
Lowassa anayewakilisha pia muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya Chadema, NLD, NCCR-Mageuzi na Chama cha Wananchi (CUF), aliyasema hayo jana mbele ya maelfu ya wananchi waliojitokeza kusikiliza kampeni zake kwenye viwanja vya Mashujaa mjini hapa jana.
Alisema kwa kuanzia, ataunda tume ya kuchunguza upya mikataba ya gesi na mafuta.
Lowassa aliongeza kuwa anafahamu kiu ya wananchi wa Mtwara kuhusiana na namna wanavyokerwa juu ya kunufaika na rasilimali hizo ambazo ni chachu kubwa ya maendeleo kwa wananchi na taifa kwa ujumla na pia ndoto yao ya kutaka wanufaike na rasilimali hizo.
Alisema wakazi wa Mtwara na Watanzania kwa ujumla, hawapaswi kuwa maskini kutokana na kuwa na rasilimali nyingi kama gesi na mafuta na kwamba akiingia madarakani atahakikisha maisha ya kila mwananchi yanapiga hatua za kimaendeleo katika kila nyanja.
“Kama mkinichagua, kila Mtanzania atanufaika... kama alikuwa anakula milo miwili basi iongezeke na kuwa mitatu. Na kama anamiliki gari moja basi awe na magari mawili. Nataka kuwa Rais wa nchi hii kwa sababu nimechoshwa na umaskini wa taifa na wananchi wake,” alisema Lowassa.
Kadhalika, Lowassa alirudia pia ahadi yake ya kuwaboreshea mazingira mazuri ya kazi madereva wa bodaboda na wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu kama machinga na kina mamalishe.
Wote hao aliwatambulisha kuwa ni marafiki zake na kwamba iwapo atachaguliwa kuwa Rais, atahakikisha hawabughudhiwi katika kazi zao bali wanasaidiwa ili nao wainuke kiuchumi.
Alisema anafahamu ugumu na changamoto wanazokumbana nazo ambazo kwa kiasi kikubwa zinachangiwa na serikali iliyopo madarakani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), akisisitiza kuwa wahifadhi vizuri shahada zao za kupigia kura na kujitokeza kwa wingi kumchagua ili awatumikie.
Sumaye amvaa magufuli
Awali, Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye alimtaka mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli, ahamie Ukawa na kuendelea na kampeni za kuing’oa CCM madarakani kwani yaelekea ananogewa na kampeni zao na ndiyo maana hutumia misemo yao, ikiwamo kubadili “Movement for Change’ (M4C) ya Chadema kuwa ‘Magufuli for Change’.
Shughuli za simama
Katika hatua nyingine, shughuli mbalimbali za biashara katika Soko Kuu la Manispaa ya Mtwara Mikindani na maeneo mengine zilisimama kwa muda jana baada ya wafanyabiashara kuamua kwenda kwenye viwanja vya Mashujaa kusikiliza sera za Lowassa na Ukawa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kabla ya kufanyika kwa mkutano huo, baadhi ya wafanyabiashara hao walisema kutokana na wanunuzi wengi kuwa katika mkutano huo, wao hawana sababu ya kukaa katika biashara zao ila ni kuungana na wananchi wengine kwenda kumsikiliza Lowassa.
Akizungumzia hali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Halima Dendegu, alisema kwa kuwa ni maamuzi ya wafanyabiashara wenyewe kusitisha shughuli zao, hakukuwa na sababu ya kuwazuia.
Dendegu alikaririwa akisema katika kituo kimoja cha redio mjini hapa kuwa mtu akisitisha biashara kwa hiari yake hakuna tatizo, bali kama kuna shinikizo lolote kutoka miongoni mwao, sheria huchukuliwa dhidi ya wahusika.
Kabla ya kutua Mtwara mjini jana, Lowassa alifanya mikutano ya kampeni pia kwenye maeneo ya Newala na Tandahimba.
Chanzo: Mpekuzihuru

Download App Yetu MPYA  >> BOFYA HAPA << Tukutumie Habari na Burudani Zote FASTA Kila Siku !

No comments

TOA MAONI YAKO HAPO CHINI.