ONE TO ONE: JOH MAKINI TUSIFANYE MUZIKI KWA MAZOEA. - BongoSwaggz.Com

Advert

Breaking News

ONE TO ONE: JOH MAKINI TUSIFANYE MUZIKI KWA MAZOEA.

Joh-makiniStaa wa Hip Hop nchini John Simon ‘Joh Makini’.
KATIKA ‘gwanda’ lake la kupigia kura, Oktoba, mwaka huu limeandikwa John Simon, lakini mashabiki wengi wa muziki, hususan Hip Hop, Bongo na Afrika Mashariki wanamtambua kama Joh Makini.
Staa huyo anayetokea Arusha, kwa sasa ndiyo habari ya mjini kwa upande wa Hip Hop akitokea Kundi la Weusi lenye vichwa kama Nikki wa Pili, Bonta, G. Nako na Lord Eyez.
Miongoni mwa nyimbo zinazoendelea kumuweka hewani na kumuingiza katika vinyang’anyiro mbalimbali vya tuzo ni Xo, I See Me na nyingine nyingi.
Wiki moja iliyopita kulikuwa na hafla fupi ya utoaji Tuzo za Kili Music iliyofanyika ndani ya Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar na kati ya wasanii waliong’ara siku hiyo ni pamoja na Joh Makini.
Joh alifanikiwa kuibuka kidedea kwa upande wa Hip Hop baada ya kuzoa tuzo mbili ambazo ni Mtunzi Bora wa Mwaka Hip Hop na Msanii Bora wa Hip Hop.
Amani lilifanikiwa kuzungumza na Joh anayebamba kwa sasa na wimbo mpya wa Nusunusu kisha akaelezea hisia zake juu ya tuzo hizo na mipango yake kimuziki.
Kabla ya KTMA, ulishiriki Tuzo za Watu ilikuaje?
“Nilichaguliwa kama mshiriki ingawa sikubahatika kushinda, ila nashukuru Mungu baada ya wiki kadhaa nikaibuka kidedea kwa kunyakua tuzo mbili za KTMA.”
Unazungumziaje ushindi wako?
“Nilistahili lakini ni jambo jema sana kwa Kampuni ya Weusi.”
Nini siri ya wewe kuwepo katika tuzo mbalimbali?
“Yapo mambo mengi sana lakini tungo, video nzuri zenye ubora, uwakilishaji wa muziki kwenye jukwaa, kampuni nzima ya Weusi pamoja na mimi mwenyewe ndiyo vimefanya kunyakua tuzo. Ujue Weusi kila msanii ndani ya wiki unatakiwa uwe na wimbo mpya. Kwa hiyo tunafanya kazi kikwelikweli.”
Unawaambia nini mashabiki wako?
“Nimewakubali, wana mihemko, wamejitolea na kuheshimu kile Joh Makini na Weusi tunafanya na ndiyo maana wakanifanya kuwa mshindi. Na ushindi wangu ni hamasa kwa wasanii wengine wanaotaka kufika mbali kisanaa, kwani tuzo ni kitu kikubwa kwa msanii.”
Unauzungumziaje Wimbo wa Nusunusu?
“Sikuwa na mpango wa kufanya video ya wimbo huo ila nilikuwa na ratiba ya kufanya video ya wimbo wangu mwingine uitwao Am On Ma Way kwa kumshirikisha msanii toka Nigeria (jina kapuni).
“Dakika za mwisho, jamaa alipata udhuru na kumfanya asifike Sauz na taarifa nilichelewa kuipata nikiwa najiandaa kwenda Sauz, hivyo sikuona sababu ya kughairi zaidi ya kwenda na ndipo nikaamua kufanya video ya Wimbo wa Nusunusu na ninamshukuru Mungu wimbo huo umepenya kimataifa na umefanikiwa kushika nafasi ya tatu katika chati ya Nyimbo Kumi Bora za  Afrika.”
Umeoa?
“Naomba hayo mambo tusiyazungumzie kwa sasa, muda ukifika kila kitu kitakuwa wazi.”
Unaamini kuna bifu kati ya Diamond na Ali Kiba?
“Sina uhakika sana na hicho kitu zaidi ya kusikia tu kwenye vyombo vya habari. Cha msingi ni wasanii kushirikiana. Bifu, makundi na vingine kama hivyo havijengi sanaa yetu bali vinabomoa na kufanya tusifike mbali. Wao wenyewe wanatakiwa wakemee siyo mpaka watoane damu.”
Mashabiki wategemee nini kwa Weusi?
“Wategemee ubora zaidi na tunawasihi wasanii wenzetu waache kufanya muziki kwa mazoea, wafanye kazi za ukweli zikaonekana na kukubalika.”
-gpl

Download App Yetu MPYA  >> BOFYA HAPA << Tukutumie Habari na Burudani Zote FASTA Kila Siku !