Advert

Breaking News

Necta: Hakukuwa na "Mazombi" Mwaka Jana, Messi

Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Charles Msonde

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani (Necta), Dk. Charles Msonde, amesema watahiniwa waliofanya mtihani wa kidato cha nne, Novemba, mwaka jana, hawakuandika vitu visivyotakiwa au kuchora ‘mazombi’ na Messi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, ingawa baadhi yao walijaza vitu visivyoeleweka.

Kwenye mitihani ya taifa iliyopita, baadhi ya wanafunzi walikuwa wakiandika mashairi ya nyimbo za muziki wa kizazi kipya kwenye karatasi za majibu na wengine kuchora vitu mbalimbali ikiwa pamoja na mfano wa picha ya mchezaji wa Barcelona, Lionel Messi, na picha nyingine za kutisha maarufu kama ‘zombie’.

Dk. Msondo aliiamba Nipashe kuwa: “Watahiniwa wamejibu kadri ya uwezo wao ulivyowatuma. Kwa mwaka huu hatujabaini watu ambao wameandika, mazombi wala freemason.

“Tunachokiona ni kwamba watahiniwa walioshindwa wanaandika majibu ambayo hayana uhusiano kabisa na baadhi ya maswali waliyoulizwa. Hawa ndio wengi wamepata sifuri na wengine alama za chini kabisa,” alisema Dk. Msonde na kuongeza:

“Ukiangalia watahiniwa waliofanya mitihani mwaka huu ni wengi kidogo. Wako 433,633 ukipata watu kama 20 wameandika hayo mambo yasiyoeleweka kwa kweli si idadi ya kutisha.

“Tunachofurahi ni kwamba walijibu. Ile ni hatua moja, wanajibu, wanaandika, hata kama majibu hayaelezi kile kilichotakiwa ni faraja, unapata picha kwamba hawa watu wamekosa maarifa, stadi na uelewa wa mada zile. Wamejibu kama walivyopata majibu kwa wakati huo.”

Alisema kazi wanayofanya kwa sasa ni uchambuzi wa kina wa matokeo ili wajue ufaulu kwa kila mada, kila mtahiniwa na kila swali ulikuwaje na baada ya hapo watatoa machapisho ya kupeleka kwa walimu.

Akijibu juu ya ufaulu wa hesabu kuendelea kuwa wa chini, alisema wanachokiona ndiyo kitu kinachoendelea darasani.

“Kwa huu ufaulu hata ukisema ule wa mwaka 2014 wa asilimia 19.58 na asilimia 16.76 ya mwaka huu (2015), tafsiri yake inakwambia kwamba tunao watahiniwa zaidi ya asilimia 80 ambao wanashindwa somo hili. Hali hii si nzuri.

“Tukiangalia Historia ni kwamba ufaulu wa hesabu kwa miaka mingi umekuwa chini. Hii inaonyesha darasani kuna kitu kinachotakiwa kufanyiwa kazi. Ukiona ufaulu uko chini au uko juu, ni kiashiria kinachojiri darasani. Kupanda au kushuka kwa ufaulu ni kiashiria ya kile mwalimu anachofanya darasani, uongozi wa shule, wazazi, walimu, wanafunzi, mkoa wilaya wanavyoshirikiana.”

“Je, walimu wana ari? Wapo wa kutosha? Wana maarifa, wanatekeleza majuku yao kikamilifu? Wanahamasisha vijana? Au wanakatisha tamaa? Watoto wana utayari wa kujifunza? Kama walimu na wanafunzi wako vizuri, uongozi wa shule? mkuu wa shule, kamati za shule, wazazi, wanashirikina vizuri?” alihoji Dk. Msonde

Akizungumza matokeo ya mwaka huu kushuka kidogo ilhali tangu 2013 yalikuwa yakiongezeka, Dk. Msonde alisema: “Sisi kitaalamu kushuka kwa asilimia 0.8 si kushuka. Ingawa bado sisi kama baraza ni vigumu kusema kwa nini umeshuka kidogo, ila kwa haraka haraka ni idadi ya watahiniwa, 433,633 waliofanya mtihani mwaka 2015, ukilinganisha na mwaka 2014 ambao walikuwa 288,247, hivyo kwa haraka kuna kundi la zaidi ya 150,000 limekuja hapa.”

Alisema kwa kawaida watahiniwa wa kidato cha nne hawajawahi kuwa 200,000 lakini kwa sababu wengi walipunguzwa 2012, walioweza kufanya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2014 walikuwa wachache.

“Kitendo cha watahiniwa zaidi ya 400,000 na matokeo yakabaki palepale, nasema ufaulu umeimarika, ndiyo maana ukisema ubora wa ufaulu daraja la kwanza mpaka la tatu, bado watakuwa ni wengi kuliko mwaka jana.

-NIPASHE
Jiunge Nasi  >> Facebook <<  >> Instagram << na >> PlayStore << Kupata Habari na Burudani Fasta Kila Time.

No comments

TOA MAONI YAKO HAPO CHINI.